About Me

header ads

Dkt. Nsekela: Shahada ya Uzamivu Inayoakisi Mageuzi ya CRDB

Na Mwandishi Wetu, Pretoria

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Mussa Nsekela, ametunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA), hatua inayotafsiriwa kama ushahidi wa namna taaluma, utawala bora na uongozi wa kimkakati vinavyoweza kuibadilisha taasisi ya kifedha na kuleta matokeo chanya ya biashara.

Dkt. Nsekela alihitimu shahada hiyo Juni 12, 2026, baada ya kukamilisha utafiti uliochambua uhusiano kati ya utawala wa makampuni na ufanisi wa kifedha wa benki za Afrika Mashariki, huku ukitathmini athari za uvujaji wa taarifa katika utendaji wa taasisi za fedha.

Utafiti huo umebainisha kuwa mifumo imara ya utawala, uwazi katika utoaji wa taarifa na udhibiti wa taarifa nyeti huongeza imani ya wawekezaji, kuimarisha utendaji wa kifedha na kuweka msingi wa ukuaji endelevu wa taasisi.
Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Dkt. Nsekela alisema kujifunza ni safari endelevu inayowasaidia viongozi kufanya maamuzi bora na kuimarisha utendaji wa taasisi wanazoongoza.

"Usimamizi makini wa makampuni si suala la nadharia pekee, bali ni msingi wa utendaji bora na mafanikio endelevu katika sekta ya fedha. Safari hii imeniongezea maarifa yatakayochangia zaidi katika kuendeleza taasisi na sekta yetu," alisema.

Mafanikio hayo ya kitaaluma yanakuja wakati Benki ya CRDB ikiendelea kushuhudia ukuaji mkubwa chini ya uongozi wake tangu alipoteuliwa mwaka 2018. Katika kipindi hicho, bei ya hisa za benki imeongezeka kutoka Sh95 hadi kufikia takribani Sh3,000 kwa hisa, huku faida baada ya kodi ikiongezeka kutoka Sh bilioni 64.1 hadi Sh bilioni 728.6 mwaka 2025.
Benki hiyo pia imefanikiwa kuharakisha mageuzi ya kidijitali, ambapo zaidi ya asilimia 98 ya miamala yake hufanyika kupitia majukwaa ya kidijitali. Idadi ya wateja imeongezeka na kufikia zaidi ya milioni 7.2 wanaohudumiwa kupitia matawi, mawakala, ATM, SimBanking na huduma za intaneti.

Katika kipindi hicho, CRDB imepanua shughuli zake nje ya mipaka ya Tanzania kwa kuimarisha uwepo wake Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, sambamba na kufungua ofisi ya uwakilishi Dubai ili kuvutia mitaji na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika masoko ya kimataifa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori, alisema mafanikio ya Dkt. Nsekela yanaonesha namna taaluma na uongozi makini vinavyoweza kuleta mageuzi makubwa ndani ya taasisi za biashara.

Alisema Benki ya CRDB imeendelea kuwa mfano wa mafanikio yanayojengwa katika misingi ya utawala bora, ubunifu na maamuzi yanayotokana na matumizi sahihi ya taarifa.

Mafanikio ya Dkt. Nsekela yanatoa funzo kwa viongozi wa biashara barani Afrika kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika maarifa na kujifunza kila wakati ili kujenga taasisi imara, zenye ushindani na uwezo wa kuhimili mabadiliko ya mazingira ya biashara duniani

Post a Comment

0 Comments