Na. Jawadu Kinyobwa – Mtwara
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb), amewataka wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kutumia maarifa, ujuzi na stadi walizopata chuoni kuchangia maendeleo ya Taifa na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.Akizungumza wakati wa Mahafali ya 43 ya Chuo TPSC Kampasi ya Mtwara, yaliyofanyika leo Juni 13, 2026, Mhe. Kikwete amewapongeza wahitimu 1,926 waliohitimu katika ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada ya Kwanza kwa juhudi, nidhamu na uvumilivu uliowawezesha kufikia mafanikio hayo.
Alisema kuwa kuhitimu masomo si mwisho wa kujifunza bali ni mwanzo wa safari mpya ya kuitumikia jamii na Taifa, huku akiwataka wahitimu kuwa mabalozi wazuri wa Chuo kwa kuzingatia maadili, uwajibikaji, uzalendo na ubunifu katika maeneo yao ya kazi na maisha ya kila siku.
“Taifa linahitaji wataalamu wenye uwezo wa kutatua changamoto, kuleta ubunifu na kuongeza tija katika sekta za umma na binafsi. Maarifa mliyoyapata yanapaswa kutafsiriwa katika matendo yenye manufaa kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” alisema Mhe. Kikwete.
Aidha, Waziri Kikwete alisema Tanzania inaelekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inahitaji wataalamu wenye maarifa na umahiri wa kutekeleza maeneo mbalimbali ya kimkakati. Alieleza matumaini yake kuwa wahitimu hao watakuwa sehemu ya nguvu kazi itakayochangia kufikiwa kwa malengo ya dira hiyo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete alipongeza Chuo kwa kuendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa mafunzo kupitia mifumo ya mtandaoni, hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa elimu kwa makundi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika taasisi zake ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za utoaji huduma na kupanua wigo wa huduma kwa wananchi.
Kuhusu tafiti, Waziri Kikwete alisema Serikali inatambua umuhimu wa tafiti zenye ubora katika kutoa suluhisho la changamoto za maendeleo na kusaidia kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi. Hivyo, aliitaka Menejimenti ya Chuo kuendelea kuimarisha shughuli za utafiti ili ziwe na mchango mkubwa zaidi katika maboresho ya sera, mifumo na huduma za umma.
Pia alipongeza juhudi za Chuo katika kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, akitaja ushirikiano na Kenya School of Government pamoja na National School of Government ya Afrika Kusini kuwa sehemu ya hatua zinazochangia kuboresha ubora wa mafunzo na kuongeza hadhi ya taasisi hiyo.
Aidha, alitoa wito kwa waajiri wote wa umma kuhakikisha watumishi wapya wanapelekwa kwenye Mafunzo Elekezi ya Awali kwa mujibu wa taratibu za Serikali ili kuwajengea uelewa wa maadili, misingi, kanuni na utamaduni wa utumishi wa umma.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Kikwete aliwataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kuleta mabadiliko chanya katika jamii, kuwa wachapakazi, wazalendo na waadilifu, huku akiwapongeza wahitimu, uongozi wa Chuo, wahadhiri, watumishi, wazazi na walezi kwa kufanikisha Mahafali ya 43 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.
Awali akitoa salaam za pongezi, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi Awali, amevitaka vyuo vya elimu ya juu kuhakikisha vinaandaa wahitimu wenye maarifa, ujuzi na umahiri unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, ili waweze kushindana na kuchangia ipasavyo maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Ernest Mabonesho amesema mazingira ya sasa ya utumishi wa umma yanahitaji matumizi ya teknolojia za kidijitali, akili bandia (AI) na mifumo ya maamuzi inayozingatia ushahidi wa kisayansi ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
"Kutokana na mabadiliko hayo, Chuo kimeendelea kuboresha mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia teknolojia za kisasa, kwa lengo la kuzalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi na stadi zinazowawezesha kuajiriwa, kujiajiri na kutoa mchango chanya katika maendeleo ya Taifa kupitia soko la ajira la ndani na kimataifa."Kuzingatia maadili ya umma baada ya kumaliza.





.jpeg)



0 Comments