About Me

header ads

AHMED MISANGA ATOA TAHADHARI YA MAANDALIZI DHIDI YA EL NIÑO TANZANIA

SINGIDA: Mwananchi na mamlaka nchini Tanzania zimetakiwa kuanza kuchukua hatua za mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa na mafuriko yanayoweza kuambatana na hali ya hewa ya El Niño.

Rai hiyo imetolewa na Ndugu Ahmed Misanga wakati akizungumza mkoani Singida, ambapo amesisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema ili kupunguza madhara kwa maisha ya watu, afya, mifugo na mali.

Amesema iwapo mvua kubwa na mafuriko yatatokea, maandalizi ya dharura yanapaswa kuanza kabla ya hali kuwa mbaya, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza madhara na kuokoa maisha.

Miongoni mwa hatua alizopendekeza ni kuongeza hifadhi ya chakula na maji salama, pamoja na kuhakikisha hospitali zina dawa na vifaa tiba vya kutosha na kuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa wengi endapo kutatokea ongezeko la mahitaji ya huduma za afya.

Aidha, Misanga amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kujitokeza baada ya mafuriko, huku akipendekeza kuandaliwa kwa kambi za dharura kwa ajili ya wananchi watakaoweza kuathirika.

Amesema pia ni muhimu kuandaa Mobile Health Facilities (Mobile Clinics) zitakazoweza kuwafikia wananchi katika maeneo ambayo huduma za kawaida za afya zinaweza kuvurugwa kutokana na mafuriko.

Katika hatua nyingine, ameitaka jamii na mamlaka kuhakikisha kuna maandalizi ya kutosha ya neti za mbu, mablanketi, mashuka, magodoro na matenti kwa ajili ya waathirika wa mafuriko.

Kwa upande wa uokoaji, Misanga amesisitiza kuimarishwa kwa timu pamoja na vifaa vya uokoaji, huku akitaka maeneo hatarishi yatambuliwe mapema na njia salama za uokoaji ziwekwe wazi.

Amesema mfumo wa tahadhari na utoaji wa taarifa za mapema kwa wananchi nao unapaswa kuimarishwa ili jamii iweze kuchukua hatua kwa wakati pindi kunapokuwa na dalili za hatari.

“Tanzania tusisubiri dharura itokee, tujandae mapema ili tuokoe maisha, afya, mifugo na mali za wananchi,” amesisitiza Misanga.

Akizungumzia mifugo, Misanga amesema maandalizi yanapaswa kuhusisha pia ulinzi wa mifugo dhidi ya mafuriko, magonjwa na upotevu, ikiwa ni pamoja na kuandaa maeneo salama ya kuhamishia mifugo pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa chakula, maji na dawa za mifugo.

Amesema mafuriko yanaweza kuleta changamoto mbalimbali kwa jamii, hivyo maandalizi yanapaswa kuwa ya pamoja na kuhusisha sekta za afya, chakula, maji, mifugo na uokoaji.

Amehimiza wananchi na mamlaka kuchukua tahadhari mapema badala ya kusubiri madhara yatokee, akieleza kuwa maandalizi ya wakati yanaweza kuwa hatua muhimu katika kupunguza athari za mafuriko na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi.

 

Post a Comment

0 Comments