About Me

header ads

MANYARA TANZANITE MARATHON 2026 YAENDESHA MBIO ZA HISANI, LENGO KUKUSANYA SHILINGI BILIONI 1.5

 

Manyara Tanzanite Marathon 2026, mbio za hisani zenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi na uwezeshaji wa wodi maalum ya kuwahudumia watoto njiti, zimefanyika leo katika Mji wa Babati, zikiwa na kaulimbiu “Hatua Moja, Okoa Maisha ya Mtoto Njiti.”

Mbio hizo za hisani zimeongozwa na Mgeni Rasmi kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Mwigulu Nchemba, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Sillo, ambaye amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa ubunifu wa kuanzisha Manyara Tanzanite Marathon, akieleza kuwa mbio hizo ni sehemu ya jitihada za kuchangia moja kwa moja katika kuokoa maisha ya watoto njiti.

Manyara Tanzanite Marathon 2026 inalenga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 1.5, fedha zitakazotumika katika ujenzi na uwezeshaji wa wodi maalum kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Mbio hizo zimewakutanisha wananchi na wanariadha kutoka maeneo mbalimbali, katika kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya na kuokoa maisha ya watoto njiti.

Mbio za Hisani za Manyara Tanzanite Marathon zimefanyika leo mkoani Manyara, zikihudhuriwa na watu mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya nchi pamoja na viongozi mbalimbali, huku lengo kuu likiwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto wachanga na watoto njiti.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Sillo, aliyemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio hizo, amepongeza uongozi wa Mkoa wa Manyara kwa ubunifu wa kuanzisha mbio hizo zinazolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya na kuokoa maisha ya watoto wachanga na watoto njiti.

Sillo amesema hatua hiyo ni mfano wa ubunifu unaopaswa kuigwa na maeneo mengine nchini, akisisitiza umuhimu wa kushirikisha jamii na wadau katika kusaidia kuboresha huduma za afya.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Jafari Rajabu, amesema mbio hizo zimeleta tija kubwa katika juhudi za kuokoa maisha ya watoto, akiwataka wananchi na wadau kuendelea kuunga mkono jitihada zinazolenga kuboresha afya ya watoto.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amewashukuru wadau wote walioshiriki na kuunga mkono maandalizi ya mbio hizo, akisema ushiriki wao umewezesha kufanikisha azma ya kuchangisha fedha kwa ajili ya watoto wanaohitaji huduma maalumu za afya.

Baadhi ya washiriki wa mbio hizo wamesema, pamoja na kushiriki kwa ajili ya mazoezi na kuimarisha afya zao, wameona umuhimu wa kuwa sehemu ya harakati za kuchangia maisha ya watoto wachanga na watoto njiti.

Wamesema ushiriki wao katika Manyara Tanzanite Marathon umewapa fursa ya kufanya mazoezi huku wakitoa mchango wa moja kwa moja katika kusaidia kuokoa maisha ya watoto, hivyo kuwataka wananchi wengine kuendelea kushiriki katika matukio yenye malengo ya kijamii na kiafya.




































 

Post a Comment

0 Comments