About Me

header ads

WATAFITI WABAINI SABABU ZA WAKULIMA WA TANZANIA KUSHINDWA KUNUFAIKA SOKO LA KIMATAIFA.

Na: Amina Hezron – Kilimanjaro.

Imebainika kuwa kutokuongeza thamani kwa baadhi ya mazao na kutokidhi vigezo vinavyowekwa kwenye Soko la dunia na wanunuzi wengine hususani nchi za Ulaya ndio sababu kuu ya Mazao mengi ya
wakulima nchini kutosafirishwa kuuzwa nje na kupata faida kubwa.

Hayo yamebainishwa na Prof. Reuben Kadigi ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Utafiti wa Biashaara, Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub) wakati akieleza matokeo ya jumla ya Mradi huo unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine ha Kilimo (SUA) nchini Tanzania na kwenye nchi
zingine 15 za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil.

“Wahitaji wanunuzi wa bidhaa zetu wanaenda wanabadirika wakiweka vigezo kanuni na sheria mbalimbali zinazotakiwa kuzingatiwa wakati wa uzalishaji ikiwemo uzalishaji unaolinda mazingira, haki kwa wafanyakazi kwenye kuzalisha zao hilo na mengine mengi ambayo ukiangalia kwa nchi yetu na nchi nyingi zinazoendelea hiyo inakuwa kikwazo kikubwa hivyo lazima nchi yetu tujipange kutimiza vigezo hivyo ili tunufaike”,alieleza Prof. Kadigi.

Mhadhiri na Mtafiti huyo Mwandamizi wa Uchumi Kilimo amesema masharti hayo hayaishii kwenye maneno tu kwa kusema bali wanakuja namifumo thabiti ya kufuatilia kujua kama kweli kile wanachouziwa kutoka kwenye nchi mbalimbali duniani kinafuata masharti yao yote waliyoyaweka.

Aidha amesema kufuatia changamoto hiyo nchi nyingi zinashindwa kufikia vigezo hivyo na kupelekea pale wanapokwenda kuuza kwenye mataifa hayo mazao na bidhaa zao zinakuwa na ushindani mkubwa kwakuwa kuna watu wanaojitangaza zaidi huko na wameweza kukidhi viwango hivyo vinavyotakiwa na soko.

Mtafiti huyo Mkuu wa Mradi wa TRADE HUB amesema jitihada za pamoja zinatakiwa kati ya Serikali,Wakulima na Makampuni makubwa ambayo yanasafirisha Mazao nje ya nchi kuwakingia mgongo wakulima wa Tanzania kwa kuwasaidia kufikia vigezo kwakuwa ili kutambuliwa pia kuna
gharama kubwa ambazo wakulima wadogo na vyama vya ushirika haviwezi kumudu.


Akizungumzia changamoto nyingine ya kutoongeza thamani kwa mazaokabla ya kusafirisha kwenda nje ya nchi kwa kutolea mfano zao la Kahawa amesema asilimia kubwa Tanzania inasafirisha kahwa ghafi (Green Coffee) wakati zipo teknolojia nyingi za kukaanga Kahawa na kuiongezea thamani
hali inayowafanya wakulima kupata hela kidogo huku wanaoongeza thamani kupata fedha kuliko mkulima.

“Nimefanya utafiti kuangalia zao la Kahawa duniani nimeona kuwa nchi nyingi zinauza Kahawa ghafi zinapata fedha kidogo sana na inanunuliwa na nchi ambayo haina hata mti mmoja wa Kahawa yaani hawalimi kabisa na kisha wanaongeza thamani tena ndogo ambayo ingeweza fanyika hapa
nchini lakini wanapata faida mara tatu zaidi kuliko sisi au mkulima aliyelima”, alieleza Prof. Kadigi.

Hivyo ameiomba Serikali katika jitihada kubwa inazozifanya katika kuinua kilimo na kufufua zao la Kahawa kuona namna ya kusaidia eneo hilo la uongezaji thamani kwa Kahawa ya wakulima wa Tanzania ili waweze kupata faida kubwa na kuona thamani ya zao hilo ambalo wakulima wengi
waliamua kuliacha kutokana na tatizo la bei.

Kwa upande wake Mtafiti Mkuu kutoka Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) katika Kituo cha Dunia cha Ufatiliaji wa Uhifadhi (WCMC) Prof. Neil Burgess amesema mradi huo unafanya utafiti kuangalia Biashara, Maendeleo na Mazingira ya mazao ya Kilimo na Wanyamapori
katika nchi washiriki.

“Huu ni mradi wa utafiti wa kimataifa unaoangalia sera za kimataifa za biashara, Usimamizi wa bishara na Kanuni za biashara lakini pia faida na hasara za kanuni zilizowekwa kimataifa kwenye biashara mfano mzuri ni hizi za Umoja wa Ulaya ambazo zinaonekana kuathiri nchi nyingi zinazoendelea”, alifafanua Prof. Burgess.

Amesema kuwa kwa Tanzania kazi kubwa imefanywa na watafiti wa SUA kupitia Mradi huo kwa miaka mitatu na sasa mwaka wa nne wanamalizia kwa kuendesha Warsha ya uhamasishaji kwa wadau pamoja na
kutengeneza muelekeo wa pamoja wa namna ya kuzalisha na kufanya biashara kimataifa sambamba na biashara uendelevu ya Nyama Pori.

Mtafiti huyo mkuu amesema kazi field na kukusanya taarifa zimemalizika na sasa wameweka nguvu katika kuandika matokeo kwa kufanya utambuzi wa kina ili kupata kitu ambacho kitakuwa na faida kutumika kwa taifa, Watunga sera na Wakulima ambao wanaguswa na mifumo mbalimbali ya
uzalishaji.

Mradi wa Utafiti wa Biashara,Maendelo na Mazingira (TRADE Hub)ni mradi wa miaka mitano unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana Taasisi zingine zaidi ya 50 duniani na kutoka katika nchi 15 za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil na kufadhiliwa
na Mfuko wa Utafiti wa Changamoto za Kidunia wa Serikali ya Uingereza (UKGCRF) na Mfuko wa Pamoja wa Utafiti na Ubunifu (UKRI).
Picha ya pamoja ya wadau wa Soya,Kahawa,Sukari na Wanyamapori kutoka taasisi za serikali na Binafsi nchi nzima walioshiriki warsha hiyo ya kupokea matokeo na kutoa mawazo yao ili kuboresha
mandiko ya mwisho ya matokeo.

Mtafiti Mkuu kutoka Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) katika Kituo cha Dunia cha Ufatiliaji wa Uhifadhi (WCMC) Prof. Neil Burgess akitoa wasilisho la Mradi kwa ujumla wake kwa nchi zote 15 washiriki.







Pich zingine ni Wadau hao wakifuatilia matokeo wakati wa warsha hiyo.Prof. Reuben Kadigi ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Utafiti wa Biashaara, Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub) kwa upande wa Tanzania wakati akieleza matokeo ya jumla ya Mradi mbele ya wadau wa mazao yaliyokuwa yanafanyiwa utafiti na mradi huo.



Post a Comment

0 Comments