


Rais Samia Suluhu Hassan amesema Shahada ya Uzamivu ya Heshima (Honoris Causa) aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi- (RUDN University) nchini Urusi, maarufu kama Patrice Lumumba University ni heshima kubwa kwake binafsi na kwa taifa la Tanzania kwa ujumla.
Akihutubia baada ya kutunukiwa shahada hiyo Rais Samia amesema katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ni muhimu kwa nchi kuwekeza katika wataalamu waliobobea ambao wanaelewa kuwa ujuzi wao ni chachu ya maendeleo endelevu ya taifa.
Ameongeza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya elimu, utafiti na teknolojia ili kuhakikisha vijana wanapata maarifa yatakayowezesha kushindana katika soko la ajira la kimataifa na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
Rais Samia ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima na Chuo Kikuu cha RUDN, kwa kutambua mchango wake katika uongozi bora, diplomasia na maendeleo ya jamii.
Shahada hiyo imetolewa wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais Samia nchini Urusi, ambapo amekuwa akifanya mazungumzo ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi.

0 Comments