Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Jeshi la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu wawili katika matukio mawili tofauti yaliyosababisha kifo cha mtu mmoja na wafugaji wanne kujeruhiwa.
Katika tukio la kwanza, Godfrey Killu (30), mkulima mkazi wa Mbwate, Mkuza, anakabiliwa na tuhuma za mauaji ya mke wake Elizabeth Sindakila (26) katika Wilaya ya Kibaha.
Tukio hilo lilitokea baada ya ugomvi kati ya wanandoa hao, ambapo Killu alimpiga mkewe kwa fimbo, hali iliyosababisha majeraha makubwa na hatimaye kifo chake.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Salim Morcase (ACP), alisema Disemba 1, majira ya saa 5 asubuhi, mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi alitoa taarifa kuhusu Elizabeth aliyefariki akiwa anapatiwa matibabu na kuwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
Anasema baada ya uchunguzi wa awali, Jeshi la Polisi lilimkamata Killu, ambaye alikiri kuhusika na tukio hilo.
Salim alieleza, mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini kwa uchunguzi wa kitabibu, na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Katika tukio jingine, mwekezaji wa kilimo Kenneth Amoni anashikiliwa kwa tuhuma za kuwajeruhi wafugaji wanne kwa risasi katika eneo la Samarogo, Kata ya Kiwangwa.
Kamanda Salim alieleza kuwa mwekezaji huyo, anayemiliki shamba la mbogamboga lenye ukubwa wa hekari 1,200, alichukua hatua hiyo baada ya migogoro iliyotokana na mifugo ya wafugaji kuingia shambani kwake.
"Kati ya majeruhi hao, mmoja amejeruhiwa paji la uso, wengine tumboni, mkononi, na begani, Wote wamekimbizwa hospitalini kwa matibabu, na mmoja amepelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi," alisema Kamanda Salim.
Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa jamii kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kusuluhisha migogoro kwa njia ya amani na kufuata taratibu za sheria.
0 Comments