Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze 5, Disemba,2024
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Sophia Lydenge, ameongoza askari wa kike wa wilaya hiyo kutoa msaada kwa wafungwa wanawake wanaotumikia adhabu ya kifungo kwa makosa mbalimbali katika Gereza la Kilimo Kigongoni, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Lydenge alisema msaada huo ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Alisema mtandao wa polisi wanawake wa Wilaya ya Kipolisi Chalinze uliamua kufika gerezani hapo kwa lengo la kuwasaidia wanawake hao, kwa imani kwamba msaada huo utawapa motisha ya kubadilika kitabia na kuwa mfano bora watakapomaliza kifungo chao.
Msaada uliotolewa ni pamoja na cherehani moja, mafuta ya kupaka, taulo za kike, pamoja na sabuni za kufulia na kuogea.
Aidha, Lydenge aliutaka uongozi wa gereza hilo kuhakikisha cherehani hiyo inatumika kuwafundisha wanawake waliopo gerezani ili, watakapotoka, wawe na ujuzi wa kushona, ambao utawasaidia kujitegemea.
Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Kaziro Ambros, akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Gereza la Kigongoni, aliushukuru mtandao wa polisi wanawake wa Chalinze.
Alihakikisha kuwa cherehani iliyotolewa itatumika kwa lengo lililokusudiwa—kama nyenzo ya kufundishia ushonaji kwa wafungwa wanawake, hatua itakayowasaidia kujijengea uwezo wa kuanza maisha mapya baada ya kifungo.
0 Comments