About Me

header ads

SERIKALI YAAHIDI KUKUZA SEKTA YA UTALII KUPITIA NaPA

 

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha.

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema miongoni mwa maeneo ya vipaumbele vya Wizara chini ya Mfumo wa Anwani za Makazi ni kushiriki kikamilifu katika kukuza Sekta ya Utalii nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 15 Septemba, 2024 na Bw. Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo, wakati akizungumza na washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wataalamu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Jijini Arusha.
Washiriki wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo Wataalamu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano Bw. Mulembwa Munaku (mwenye koti la Buluu Katikati) na Wataalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi tarehe 15 Septemba, 2024. 
Mafunzo hayo yamefanyika Katika jengo la Kituo cha Utalii Ofisi za Hifadhi ya Ngorongoro, Jijini Arusha.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari yameanza tarehe 12 Septemba, 2024 yakitarajiwa kuhitimishwa tarehe 16 Septemba, 2024, yana lengo la kuwawezesha wataalamu hao kuwa na ujuzi wa kutoa Anwani za Vivutio vya Utalii vilivyopo kwenye Hifadhi ya Ngorongoro.

“Maendeleo ya aina yeyote yanategemea sana utaalamu, hivyo wataalamu mnaopata mafunzo haya mnao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa, adhma ya Serikali ya kukuza utalii inachochewa kupitia matumizi ya Mfumo wa NaPA”, amesema Bw. Munaku na kuongeza kuwa;



“Kupitia zoezi hili, wataalamu mfikirie namna bora ya kuimarisha, kuchochea na kuvutia watalii wa ndani (wananchi) na watalii wa nje kwa ujumla wake”.

Kwa upande wake Mratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi Kitaifa, Mhandisi Jampyon Mbugi, amesema hatua hiyo inalenga kuongeza wigo wa kutangaza huduma na vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kuvutia watalii kutembelea maeneo hayo na hivyo kuongeza pato la Taifa.


Post a Comment

0 Comments