About Me

header ads

KAMISHNA MKUU TRA NA MKUU WA WILAYA ILALA, WAKUTANA NA MACHINGA, WAKUBALI KULIPA KODI

 


Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo leo Septemba 05, 2024 wamekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Jumuiya ya wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Taifa wa jumuiya hiyo Stephen Lusinde. Mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa TRA Dar es Salaam ambapo wamejadili mambo mbalimbali yahusuyo kodi na wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) wemesema wapo tayari kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.





Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
WAFANYABIASHARA ndogondogo maarufu kama 'Machinga mkoani Dar es Salaam wamesema wako tayari kulipa kodi kulingana na kipato wanachopata kwa mwaka.

Hatua hiyo imekuja baada ya wamachinga hao kukutana na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na kujadiliana masuala mbalimbali ikiwemo ulipaji wa kodi, namna ya kuwapanga kwenye masoko.

Akizungumza jana Dar es Salaam, mara baada ya kikao chao Mwenda amesema wana dhamana ya kuwasaidia wafanyabiashara wote waweze kuendeleza biashara zao.

Amesema kisheria wafanyabiashara wenye mauzo kuanzia Sh milioni nne hadi saba kwa mwaka wanapaswa kuchangia kuanzia Sh 100,000 sawa na Sh 8,300 kwa mwezi.

"Kwa wamachinga waliopo Kariakoo wengi wao mauzo ni zaidi ya hayo. Hivyo, tutaanza na kiwango cha Shilingi laki moja kwa mwaka. Kwa wenye mauzo kuanzia milioni saba anachangia 250,000 sawa na Shilingi 20,800 kwa mwezi," amesema Mwenda.

Alieleza kuwa baada ya kuwapanga wamachinga hao wateja wataamua kwenda kununua bidhaa kwa wamachinga au Kariakoo kwani wamachinga hao wako tayari kulipa kodi hivyo wataendelea kutoa elimu ili wale wanaostahili kulipa kodi wafanye hivyo.

Mwenda ameongeza kuwa, wamekubaliana namna ya kuwapanga vizuri bila kuathiri wafanyabiashara hao na wale wakubwa ili soko la Kariakoo liendelee kuwa soko la kimataifa.

"Tutatengeneza kamati ya pamoja itakayohusisha wataalamu kutoka TRA, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili kuwapanga kwa muda mfupi na mrefu na kujenga ushirikiano baina yao na wale wenzao ambao wapo Kariakoo wakati tunatafuta ufumbuzi ili kila mmoja afanye biashara bila kuathiri wengine."

Amesema, wamachinga wapo tayari kutoa taarifa za wakwepa kodi na kwamba watahakikisha wanawasaidia mpaka pale watakapokuwa walipa kodi rasmi.

"Rais alituagiza tutafute namna bora na shirikishi ya kuwapanga, kuongeza idadi ya walipa kodi na tunaamini wapo wamachinga wengine ambao wanapata mauzo ya Shilingi milioni nne kwa mwaka hivyo tukiwatambua na kuwasajili tutaongeza idadi ya walipa kodi na kurasimisha sekta isiyo rasmi ," alisema

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Tanzania na Mwenyekiti Soko la Kariakoo, Stephen Lusinde amesema kuwa wamachinga wote wako tayari kulipa kodi ambayo itaendana na uwezo wao.

Amesema kulipa kodi ni uzalendo kwani maendeleo yanayofanywa nchini yanatokana na kodi za Watanzania hivyo, hawako tayari kuona maendeleo bila mchango wa wamachinga.

Amesema wataanza kutoa elimu ya pamoja kuhusu ulipaji wa kodi na kwamba itawafanya wawe sekta rasmi kwa kuwa wanalipa kodi ya serikali na kuchangia kwenye ujenzi wa taifa.

Lusinde amesema kuwa yapo masoko mengi yaliyojengwa lakini hayana miundombinu ambayo ni rafiki kwa wamachinga hivyo kuchangia kurudi katika maeneo yasiyo rasmi.

"Tunaomba mamlaka zije na mipango mizuri ya kuwapanga wamachinga Kariakoo ikiwemo kuweka kanuni kwani kuna mitego imewekwa ili wamachinga waondoke na wao wageuze soko, sisi tuko tayari kulipa kodi na tutakuwa wa kwanza kuonesha uzalendo kwa nchi yetu," amesema Lusinde.

Pia alisema hawako tayari kuwalinda walipa kodi ili kusiwepo na visingizio kwamba wafanyabiashara wakubwa hawalipi kodi kwa sababu yao.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema, mkakati wao ni kuhakikisha Soko la Kariakoo linabaki kuwa la kimataifa kwa kuhakikisha hakuna wamachinga watakaokaa kwenye njia za kuingilia sokoni hapo.

Amesema masoko katika maeneo mbalimbali yanajengwa ili wamachinga wapate eneo la kufanyia biashara hivyo, wataongeza idadi ya walipa kodi.

"Tunawatengenezea mazingira wamachinga kwani pia wana mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi, pia lazima tuwaheshimu wafanyabiashara wakubwa," amesema Mpogolo.

Post a Comment

0 Comments