Na. Saidina Msangi, Chalinze, Pwani.
Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze wameishukuru Serikali kwa kuwafikishia elimu ya fedha itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi kwa kutumia fursa za uwekezaji ili kujiongezea kipato na kuongeza thamani ya akiba zao.
Wananchi hao walitoa shukrani hizo baada ya kupata mafunzo ya elimu ya fedha yaliyoratibiwa na Wizara ya Fedha, yenye kauli mbiu "Elimu ya fedha ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi" ambayo yametolewa kwa siku mbili katika ukumbi wa mikutano wa Wilaya ya Halmashauri ya Chalinze.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake, Bi. Mery Leonard Chiwiko, aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapa elimu hiyo muhimu, akisema kuwa hapo awali hawakuwa na uelewa mzuri kuhusu masuala ya fedha, mikopo na uwekezaji.
"Tunaishukuru Wizara ya Fedha kwa kutupatia elimu hii, itatusaidia sana katika kuimarisha maisha yetu ya kifedha, kuepukana na mikopo umiza na pia tumejifunza kuwa hata kama una kipato kidogo inawezekana kuweka akiba na kuwekeza akiba hiyo na kupata faida," alisema Chiwiko.
Wananchi hao waliiomba Serikali kuona namna ya kuwafikishia mafunzo ya elimu ya fedha ikiwezekana mara mbili kwa mwaka kutokana na umuhimu wake katika kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kiuchumi.
Timu ya Maafisa kutoka kutoka Wizara ya Fedha imetoa mafunzo ya elimu ya fedha ikiwemo namna ya kuweka akiba na mbinu za usimamizi wa fedha na uwekezaji kwa washiriki zaidi ya 800 ambao wanatarajiwa kuwa mabalozi wa kuwafikishia wenzao elimu hiyo ili nao waweze kunufaika na kujikwamua kiuchumi.
Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi wa Wizara ya Fedha, Bi. Mary Mihigo, akitoa elimu ya fedha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa usimamizi wa fedha binafsi, jinsi ya kupanga mapato na matumizi ili kuweka akiba na kujikwamua kiuchumi pamoja na kujiandaa na maisha ya baadaye, wakati Maafisa wa Wizara ya Fedha walipokuwa wakitoa elimu ya fedha kwa wananchi katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Chalinze.
Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi wa Wizara ya Fedha, Bi. Mary Mihigo, (mwenye sare), akijadiliana na wananchi mbinu za kuhakikisha mikopo wanayochukua ni salama kwa kuzingatia taasisi za watoa huduma za fedha zilizosajiliwa, wakati Maafisa wa Wizara ya Fedha walipokuwa wakitoa elimu ya fedha kwa wananchi, katika Kata ya Kiwangwa, Halmashauri ya Chalinze.
Afisa Masoko na Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko wa Uwekezaji wa UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akiwaelekeza wananchi kuhusu mifuko ya uwekezaji inayopatikana katika Mfuko wa Uwekezaji wa UTT Amis na jinsi wanavyoweza kunufaika na fursa za uwekezaji, wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha iliyotolewa na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Chalinze.
Afisa Maendeleo ya Jamii na Msajili Msaidizi Vikundi vya Huduma Ndogo za Fedha, Halmashauri ya Chalinze, Bi. Flora Barakana, akitoa ufafanuzi kwa wananchi waliohudhuria katika programu ya utoaji elimu ya fedha kwa wananchi inayotekelezwa na Wizara ya Fedha, kuhusu namna ya kusajili vikundi na kuwawezesha kupata fursa ya mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Serikali, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Chalinze.
Baadhi ya wananchi wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha waliowasili kutoa elimu ya fedha kwa wananchi, kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, dhamana za mikopo, riba pamoja na uwekezaji, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Chalinze. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Chalinze, Pwani)
0 Comments