About Me

header ads

RITA YASAJILI ZAIDI YA WANANCHI 5,000 KATIKA MAONESHO YA SABASABA 2024

 
WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) yasajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi zaidi ya 5,000 katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama SabaSaba.

 Akitoa taarifa hiyo kutoka katika banda la RITA viwanja vya SabaSaba, Afisa msajili wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ,Mariam Ling'ande amesema kuwa safari hii wananchi wengi wameonesha kuwa na muitikio mkubwa wa kufuatilia vyeti vya kuzaliwa na hii ni kutokana na kujua umuhimu wa kuwa na cheti hicho ili kujipatia mahitaji muhimu katika jamii yetu.

 

Aidha, wananchi wameipongeza RITA kwa huduma ambayo wameitoa katika maonesho hayo bila ubaguzi wowote na bila usumbufu ambapo kila aliyehitaji huduma ya cheti cha kuzaliwa alipewa.

 

Pia, amesema RITA iko imara kwa kutoa huduma hiyo, kwasababu changamoto waliyoipata katika maonesho hayo ni watu kuwa wengi ambapo hatahivyo waliweza kuhakikisha kuwa kila aliyefika katika banda la RITA alipata huduma stahiki.

"Changamoto tuliyoipata ni watu kuwa wengi, ambapo ikasababisha huduma hiyo kutolewa hadi saa moja usiku, ili kila aliyefika katika banda hili aweze kupata huduma kulingana na mahitaji yake," Alisema Bi. Ling'ande

 

Mmoja wa wananchi hao aliyejulikana kwa jina la Bi.Asha Mussa ameipongeza RITA kwa huduma ambayo wameitoa na yeye kuweza kufanikiwa kupata cheti chake cha kuzaliwa kwa gharama nafuu na kwa haraka.

 

Amesema "kwakweli wananchi tulikuwa wengi sana ambao tunahitaji huduma ya vyeti, lakini tulipokelewa vizuri na maafisa wa RITA  waliokuwa wanatoa huduma na kutuhudumia kulingana na mahitaji yetu,naipongeza sana RITA kwa kutuletea huduma hii kwenye maonesho haya makubwa"

 

Naye, Bwana Emmanuel Masanika amesema kuwa, hakuwahi kutegemea kupata cheti cha kuzaliwa kulingana na umri wake kutokana na baadhi ya wananchi huko mtaani kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu ugumu wa  kupata huduma hiyo, lakini mara baada ya kufika katika banda hilo alipewa maelekezo na kisha kuanza hatua za kupata cheti tofauti na alivyodhani hapo awali.


 "Tunashukuru kupata huduma hii hapa hapa sabasaba, Mimi ni mkazi wa Chanika kwangu ilikuwa rahisi kufika hapa kwa sababu kila nilipotamani kuifuata huduma hii katika ofisi zao nilikuwa naona uvivu kwa kuona  kuwa ni mbali," amesema Masanika. 












Kama inavyoonekana pichani  Maafisa wa RITA wakiendelea na kazi ya kuwahudumia wananchi.(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MASSAKA, MICHUZI TV)

 

Post a Comment

0 Comments