About Me

header ads

Benki ya NBC Yazindua Kadi Uanachama Msalaba Mwekundu, Dkt Biteko Aguswa na jitihada zake ufanikishaji miradi mikubwa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko amepongeza jitihada za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kuunga mkono jitihada za serikali katika kuongeza ujumuifu katika huduma za kifedha (financial inclusion) sambamba na kusaidia ufanikishaji wa miradi mikubwa ya kitaifa ukiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji Mkoani Tanga kupitia hati fungani ya kijani iliyosimamiwa na benki hiyo.

Dkt Biteko alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki alipotembelea banda la benki hiyo lililokuwa kwenye viunga vya ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ambapo yalifanyika Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania. Dkt Biteko alimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassani kwenye maadhimisho hayo ambayo pia yalihusisha uzinduzi wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama hicho kupitia benki ya NBC.

Akizungumza mara baada kupokea taarifa ya Meneja wa Kanda ya Kati wa benki ya NBC Miraji Msuya kuhusu jitihada mbalimbali za benki hiyo katika kuhudumia jamii ukiwemo usimamizi wa hati fungani ya kijani ya ujenzi wa miundombinu ya maji Mkoani Tanga na utambulisho wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama cha Msalaba Mwekundu, Dkt Biteko aliipongeza benki hiyo kwa jitihada hizo huku akitoa wito kwa taasisi za fedha nchini kuendelea kushirikiana na serikali kubuni huduma mbalimbali zinazolenga kuwakwamua wananchi kwenye changamoto zinazowakabili.

“Niwapongeze sana NBC kwa jitihada hizi na wito wangu kwa taasisi za fedha ni wao kuendelea kushikirikiana na serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kutatua changamoto za wananchi kama ujenzi wa miundombinu ya maji pamoja na kuendelea kuvutia wananchi wengi zaidi waingine kwenye mfumo rasmi wa huduma za kifedha,’’ alisema.

Dkt Biteko pia aliongoza zoezi la uzinduzi wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kupitia benki ya NBC akiwa sambamba na viongozi wengine waandamizi wa serikali wakiwemo mawaziri, viongozi waandamizi wa Chama cha Msalaba wakiongozwa na Rais wa chama hicho ambae pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile pamoja na maofisa wa benki hiyo wakiongozwa na Meneja wa Kanda ya Kati wa benki ya NBC Miraji Msuya.

Akizungumzia hatua hiyo Msuya alisema ni matokeo ya ushirikiano baina ya benki hiyo na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania unaochochewa na azma ya pamoja baina ya taasisi hizo mbili ambayo ni kujitolea katika kusaidia jamii kwenye masuala mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo utoaji wa misaada tofauti kufuatia athari zitokanazo na majanga mbalimbali yanayolikumba taifa.

“Ni kutokana na kushabihiana kwa dhamira baina yetu NBC na wenzetu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania ndio kumesababisha ushirikiano huu unaoshuhudiwa leo. Pamoja na kuwa sehemu wa wadau muhimu katika kufanikisha maadhimisho haya, leo benki ya NBC tunashirikiana na chama hiki kuzindua kazi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama hiki ambazo pamoja na kuwa kadi za uachama wa Red Cross pia zinawawezesha kufanya miamala mbalimbali ya kibenki,’’ alisema Msuya.

Akizungumzia zaidi faida zinazoambata na kadi hiyo kwa wanachama hao, Msuya alisema zimeunganishwa na huduma ya bima ya afya kwa wanachama inayomuwezesha mwanachama kulipwa fidia akipata ulemavu au familia yake kulipwa viwango tofauti pindi muhusika anapofariki.

“Zaidi kadi hiyo inamuwezesha mwananchama kulipia ada za uanachama, kulipia malipo mbalimbali ikiwemo ikiwemo visimbuzi vya TV na kulipia mechi za ligi Kuu ya NBC ‘’ aliongeza.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko (wa nne kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania za benki ya NBC . Zoezi hilo lilifanyika wakati wa Maadhimisho ya miaka 62 ya chama hicho yaliyofanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki. Wengine ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (wa tatu kulia), Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania ambae pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile (wa tatu kulia) na Meneja wa Kanda ya Kati wa benki ya NBC Miraji Msuya (wa pili kulia)





Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko (wa pili kushoto) akisikiliza maelezo kuhusu huduma mbalimbali za benki ya NBC kutoka kwa Meneja Mahusiano wa benki hiyo Joseph Kapinga wakati alipotembela banda la benki hiyo lililokuwa kwenye viunga vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma yalipofanyika Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania. Wengine ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (katikati), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman (wan ne kulia), Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania ambae pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile (kulia) viongozi wengine wa serikali na wafanyakazi wa benki hiyo.





Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko (pichani) akizungumza na washiriki wa Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.





Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (pichani) akizungumza na washiriki wa Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.





Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania ambae pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile (aliesimama) akisalimiana na washiriki wa Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.





Meneja wa Kanda ya Kati wa benki ya NBC Miraji Msuya (Pichani) akisalimiana na washiriki wa Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma. Benki hiyo ilikuwa moja ya wadau muhimu wa maadhimisho hayo kupitia udhamini na wa uzinduzi wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania za benki ya NBC.





Maofisa wa benki ya NBC Dodoma wakiongozwa na Meneja Mahusiano wa benki hiyo Joseph Kapinga wakionyesha mfano wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania za benki ya NBC wakati wa Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.





Baadhi ya washiriki wa Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.

Post a Comment

0 Comments