Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Jopo la Watafiti katika Mradi wa Utafiti wa Mazingira ya Chakula katika
Miji na kuboresha lishe ya Walaji (FETE) wamekutana kuzindua mradi na
kupanga mikakati ambayo itasaidia kuimarisha lishe ya jamii na kupunguza
utapiamlo kwa nchi nne za Afrika zinazoshiriki utafiti huo.
Hayo yamebainishwa na Mtafiti Mkuu wa mradi huo kwa upande wa
Tanzania Prof. Joyce Kinabo ambaye ni Profesa wa lishe wakati akitoa
utambulisho wa Mradi huo kwa jopo hilo linalohusisha watafiti kutoka
Tanzania, Ghana, Afrika ya Kusini,Malaysia na Ujerumani kwa ufadhili wa
Shirikisho la Shirika la Kilimo na Chakula la Ujerumani (BLE).
“Wengi mtakubaliana na mimi kuwa tuna matatizo makubwa ya utapiamlo
wa chini na utapiamlo wa juu kwa maana kwamba uzito ulikithiri na unene
unazidi kuwa changamoto kwa watu wengi hapa Tanzania changamoto
ambayo inachangiwa na mazingira hafifu na mabaya ya chakula”, alieleza
Prof. Kinabo.
“Vyakula vingi ambavyo tunaviona kwenye maduka yetu na supermarket
vingi ni vile vya kusindikwa na vingi vinakuwa na sukari nyingi,Mafuta
mengi na hivyo kusababisha mlaji kuchukua wanga au sukari zaidi ya
mahitaji ya mwili wake na hii humfanya mtu aongezeke uzito kwa kasi na
hivyo kupelekea kupata magonjwa yasiyo ya kuambukizwa mfano Kisukari,
Shinikizo la damu na magonjwa ya moyo”, aliongeza Prof. Kinabo.
Hivyo amesema utafiti huo unalenga kuboresha mazingira ya masoko na
maeneo yote yanayouza chakula ili waweze kuuza vyakula ambavyo
vitampatia mlaji lishe bora kama vile matunda, mbogamboga na jamii ya
mikunde na sio vyakula ambavyo vinaenda kumuongezea matatizo hasa
vilivyosindikwa sana na kuongezea sukari nyingi na mafuta mengi.
Prof. Kinabo amesema kuwa utafiti huo utatoa somo na suluhisho la nini
kifanyike kwa upande wa wadau, Sera, na wauzaji wa vyakula ili kwa
pamoja waweze kuipa jamii chakula kitakachosaidia kuimarisha lishe za
afya za watu.
Amesema Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kinanufaika hasa kupitia
wafanyakazi wake kupata ufadhili wa masomo katika shahada za Uzamivu
lakini pia wanataaluma watafiti kwenye mradi huo kupata nafasi ya
kuchangamana na wenzao kutoka nchi zingine na kuongeza uzoefu na
mashirikiano katika maeneo ya utafiti.
Akizungumzia kilichowasukuma kutekeleza mradi huo wa utafiti Mratibu
wa Mradi huo kwa nchi zote nne Dkt. Daniella Waible kutoka Taasisi ya
Uchambuzi wa Masoko ya Thenen ya nchini Ujerumani amesema ni tatizo
kubwa la utapiamlo,Ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza na hasa
zinazoathiri ukuaji wa uchumi ambapo tabia za kilishe zinapitia mabadiliko
makubwa.
“Lengo kubwa ni kuanzisha ushirikishaji wa tatizo na fursa, kuleta
suluhisho la kutengeneza mazingira bora ya chakula, kutoa mfano wa
marejeo, kutoa modeli ya marejeleo ya jinsi mbinu zilizoanzishwa na
matokeo yaliyopatikana yanavyoweza kutumika kwa upana zaidi katika
Kusini mwa dunia kwa kuwalenga watu wa hali ya chini mijini”, alifafanua
Dkt. Daniella.
Mratibu huyo wa mradi huo wa utafiti amesema andiko la mradi kwa
wafadhili liliwasilishwa toka mwaka 2019 na kupitia michakato mbalimbali
na hatimae mwezi wa 12 mwaka 2022 ndio likakubaliwa na hivyo akatumia
nafasi hiyo kuwashukuru wadau wote walioshiriki kwa uvumilivu na
michango yao ya mawazo katika kufanikisha mradi huo muhimu kwa
maendeleo ya nchi zote.
Akifungua mkutano huo Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Juu,
Utafiti na Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (DRPTC)
Prof. Esron Karimuribo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amepongeza uchaguzi wa
mada ya Utafiti huo na kwamba umekuja wakati muafaka ambapo
kumekuwa na changamoto kubwa ya ongezeko la magonjwa yasiyo ya
kuambukizwa yanayohusishwa na lishe duni.
“Tunashuhudia vifo vya watu wetu vinavyotokana na wao kutokujua
mambo ya msingi tu ambayo yanahusiana na lishe hivyo sisi kama nchi
lakini pia katika ukanda huu tunapongeza mada ya utafiti huu
mliyochangua kwakuwa inakwenda kujibu changamoto hizo ambazo
zinaathiri afya za jamii zetu”, alifafanua Prof. Karimuribo.
Hata hivyo kwa niaba ya Uongozi wa SUA, Prof. Karimuribo
amewahakikishia watafiti hao ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha
utekelezaji wa mradi na kuwaeleza kuwa wamechagua mahali sahihi
kutokana na Chuo hicho kuongoza kwa miaka mitano mfululizo kwenye
masuala ya Utafiti na machapisho nchini Tanzania hivyo wanafanya kazi na
taasisi bora nchini.
Jopo la watafiti wa Mradi huo wa FETE linajumuisha watafiti na wanafunzi
kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo nchini Tanzania,Taasisi ya
uchambuzi wa Masoko ya Thunen ya Ujerumani, Taasisi ya Utafiti wa
masuala ya Sera za Sayansi na Tenolojia (STEPRI) ya nchini Ghana, Chuo
Kikuu cha Nottingham cha Malaysia na Chuo Kikuu cha KwaZulu – Natal
cha Afrika ya Kusini.Mtafiti Mkuu wa mradi wa utafiti wa (FETE) kwa upande wa Tanzania Prof. Joyce Kinabo akizungumza wakati wa uzinduzi wa
mradi huo.
Mratibu wa Mradi huo kwa nchi zote nne Dkt. Daniella Waible kutokaTaasisi ya Uchambuzi wa Masoko ya Thenen ya nchini Ujerumani akitoa neno wakati wa uzinduzi wa mradi.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Juu, Utafiti na Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (DRPTC) Prof. Esron Karimuribo akifungua Mkutano wa uzinduzi wa mradi huo wa FETE.
Picha ya pamoja ya jopo la watafiti kutoka nchi tano zinazotekeelza mradi huo wa utafiti.
Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kwa upande wa Tanzania Prof. Joyce Kinabo (Kushoto) akipokea zawadi kutoka Ujerumani kwa niaba ya wanajopo hilo zilizokabidhiwa na Dkt. Johanna Schott.
0 Comments