About Me

header ads

VIJANA WAHIMIZWA KUJIWEKEA AKIBA KWA MANUFAA YA SASA NA BAADAYE

 

NA. Mwandishi wetu Arusha.

VIJANA nchini wamehimizwa kutumia vizuri vipato wanavyopata kujiwekea akiba ili kumudu maisha yao ya sasa na baadaye.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Hifadhi ya Jamii, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Frank Kilimba, kwenye banda la Ofisi ya Waziri Mkuu, katika Maadhimisho ya 3 ya Wiki ya Huduma ya Fedha, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Novemba 21, 2023.

Bw. Kilimba amesema, Ofisi nya Waziri Mkuu inashughulika na makundi mabalimbali yakiwemo ya Vijana, Hifadhi ya Jamii na Wenye Ulemavu na kwamba wanayatumia maadhimisho hayo kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye Ofisi hiyo.

Alisema kupitia Halmashauri, Ofisi ya Waziri Mkuu inatoa mikopo kwa vikundi na mtu mmoja mmoja kulingana mradi uliobuniwa na kijana au kikundi husika.

“Pamoja na kuwaelimisha vijana namna ya kupata mikopo, tunawaelimisha wanapoendesha biashara zao wajiwekee akiba kwa ajili ya majanga yanayoweza kutokea baadaye, hususan janga la uzee, ambapo mtu anapozeeka hawezi kufanya kazi kama ilivyokuwa hapo kabla.” Alifafanua.

Alisema mikopo inayotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea vizuri ni nafuu sana kwa vijana kujikwamua katika biashara zao.

Wakizungumza baada ya kutembeela banda hilo, vijana kutoka wilaya za Longido, Ngorongoro na Simanjiro, wamesema elimu waliyoipata imewawezesha kujua fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu na kutoa ushauri kwa Halmashauri kutoa elimu zaidi ili kuwasaidia vijana kutambua fursa hizo.

“Kupitia elimu niliyoipata nimegundua kuwa, kuna mikopo inayotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya Vijana na fedha kwa ajili ya mikopo hiyo inapitia kwenye Halmashauri zetu, mimi ningeshauri kwamba Halmashauri ziwasaidie vijana kuwapatia maelezo ya kutosha kuhusu fura ya mikopo hii ili sisi vijana wengi zaidi tuweze kufaidika.” Alisema Sera James, kutoka wilaya ya Longido.

Naye Noah Lerindo Lesirkon, kutoka Simanjiro amesema, uelewa alioupata kuhusu mafunzo kwa vijana yanayowasaidia kuwajengea ujuzi ili waweze kujiajiri.

“Programu hizi za kuwajengea uwezo vijana ili wajiajiri wenyewe zinasaidia vijana wengi ambao wamehitimu vyuo mbalimbali na wamekaa wakisubiri ajira.” Alisema.

Naye Naini Lolusu, kutoka Ngorongoro, alisema yeye ni muhitimu kutoka Chuo cha Mipango, Tabora katika fani ya Afisa Rasikimali Watu na Utawala, lakini ndoto yake ni kujiajiri kama mama ntilie na kwamba programu ya Uanagenzi ambayo inatoa ujuzi mbalili imemvutia sana.

“Mimi nimesoma Human Resources Management and Administration, lakini ndoto yangu kubwa ni kuwa mama lishe, nimepata maelekezo ya namna ya kujiunga na mafunzo ya uanagenzi ili niweze ,kupata fursa ya kupata elimu hiyo.” Alisema

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa yameanza Novemba 20, 2023 na yatafikia kilele, Novemba 26, 2023, lengo hasa likiwa ni kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutumia huduma rasmi za fedha ili kujikwamua kiuchumi na kupunguza kiwango cha umasikini nchini.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ni “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo Kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments