Wananchi, Wazazi na Walezi wa Kata ya Manyoni mkoani Singida, wakiwa kwenye mkutano ulioandaliwa na Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Kata ya Manyoni kwa ajili ya kujadili utokomezaji wa ukatili katika kata hiyo na maeneo mengine na kuanzisha kampeni ya uchangiaji wa chakula mashuleni, uliofanyika jana Juni 2,2023 Shule ya Msingi Tambukareli na kuongozwa na Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo, Shujaa, Wallece Sechambo.
.............................................................
Na Dotto Mwaibale, Manyoni
SHUJAA wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Kata ya Manyoni
mkoani Singida, wameanza kampeni ya kufa na kupona ya kuhamasisha jamii
kuchangia upatikanaji wa chakula mashuleni ikiwa ni sehemu ya mapambano ya
vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Juni 2, 2023 katika mkutano
uliofanyika Shule ya Msingi ya Tambukareli wilayani humo na kuwahusisha wazazi
na wananchi kwa ajili ya kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili na
kuanzisha kampeni hiyo, Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo, Shujaa
Wallase Shechambo alisema mikutano ya namna hiyo ya kuwahusisha wazazi na
wananchi ni ya muhimu katika mustakabari mzima wa kupinga ukatili.
"Sisi kama SMAUJATA katika kata yetu tumeona ni vizuri kufanya
mikutano ambayo tutawashirikisha wananchi, walezi na wazazi kwa lengo la kukaa
pamoja ili kuzungumzia vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia na kutafuta mbinu
za kutokomeza vitendo hivyo'" alisema Shechambo.
Alisema upo ukatili wa aina mbalimbali kama, ndoa za utotoni, ubakaji,
ukatili wa kingono, kisaikolojia, kiuchumi, kipigo, kuwanyima watoto haki ya
kwenda shule kusoma, ulawiti, ukeketaji, biashara haramu ya kusafirisha
binadamu na mwingine mwingi unaofana na
huo na kuwa kazi kubwa ya SMAUJATA ni kuupinga kwa nguvu aina zote za ukatili.
Shechambo alisema katika kata hiyo na wilaya nzima ya Manyoni kumekuwa na
vitendo hivyo na kuwa wao kama SMAUJATA wamejipanga vilivyo kupambana na
vitendo hivyo ambavyo si vizuri katika jamii na hata Mwenyezi Mungu
havimpendezi.
Shechambo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi, wazazi na walezi mara watakaona au kubaini kuwepo kwa
vitendo vyote vya ukatili kwenda ofisi ya kata hiyo au dawati la jinsia kituo
kikuu cha Polisi wilayani humo kutoa taarifa ili hatua za kisheria zichukuliwe
dhidi ya watuhumiwa.
Mwenyekiti wa SMAUJATA wa Kata hiyo, Hossen
Kheri alisema pamoja na kujadili suala la ukatili wa kijinsia pia
waliona watumie mkutano huo kuanzisha kampeni ya kuhamasisha jamii kuchangia chakula ili wanafunzi
waweze kupata chakula cha mchana wawapo shuleni kwani wamebaini baadhi ya
watoto wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili kutokana na kudanganywa kwa
kupewa pesa za kununulia chakula au kununuliwa na watu wenye nia mbaya na
kujikuta wakinaswa katika mtego huo.
"Watoto wetu wanapokosa chakula shuleni ni rahisi kurubuniwa kwa
kupewa hela kwa ajili ya kununulia chipsi na vyakula vingine hivyo shime wazazi
tujitoe kusaidia kupata chakula ili kuwanusuru kwani tukiamua jambo ili
linawezekana hakuna sababu ya kuisubiri Serikali kutufanyia suala hili,"
alisema Kheri.
Katibu wa SMAUJATA wa kata hiyo, Sara Yohana naye aliunga mkono suala hilo
la kuhamasisha wazazi kupata chakula cha watoto wakiwa shuleni na kueleza
kukosekana kwa chakula hicho kuna madhara makubwa kwa wanafunzi ikiwa pamoja na
kutozingatia vizuri masomo.
"Suala hili wala sio la kuiachia Serikali ni letu sote na njaa haina
mtu mkubwa wala mtoto na mdogo kwani ukipita muda wa kula hata mtu mzima utakuta anakuwa kimya
kwa maumivu ya njaa sembuse mtoto," alisisitiza Yohana.
Katika tukio lingine kikosi kizima cha SMAUJATA katika kata hiyo kimeweza
kuibua tukio la watoto watatu wa familia moja ambao walikuwa wakifanyiwa
vitendo vya ukatili na kushindwa kupelekwa shuleni licha ya mtoto wa kwanza
kuwa na umri wa miaka 13, wa pili miaka tisa na mdogo wao akiwa na miaka saba.
Watoto hao inadaiwa tangu wazaliwe hawajawahi kupelekwa shuleni zaidi ya
kuwepo nyumbani wakifanyiwa vitendo vya ukatili lakini jana baada ya viongozi
hao wa SMAUJATA kupata taarifa hiyo walikwenda kutoa elimu kwa wazazi wa watoto
hao kuhusu umuhimu wa watoto hao kupata elimu ambao walikiri kufanya makosa
ambapo viongozi hao walikwenda kuzungumza na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya
Tambukareli ambaye alikubali kuwapokea na mwezi ujao shule zitakapofunguliwa
wataanza kusoma kwa utaratibu atakao wapangia.
Kikosi kazi cha Mashujaa wa SMAUJATA kilichofanya kazi hiyo kubwa kikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wao Shujaa Wallece Shechambo ni Hossen Kheri, Sarah Yohana, Joyce Peter, Henry Mallya, Neema Massabuni, Zena Salum na Mary Saileni.
0 Comments