Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Dk.James Mrema (katikati waliokaa), ambaye alimuwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi hiyo, Tanzania, Profesa William Pallangyo akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chama cha Ushauri na Uelekezi kwa Washauri wa Wanafunzi Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TACOGA 1984), baada ya kufungua mafunzo yanayohusu namna bora ya kukuza utendaji katika kuwapa ushauri wanafunzi wanao walea na kuwaongoza yalioanza Juni, 21, 2023. Kutoka kushoto ni Makamu Mwenyekiti TACOGA 1984, Augustine Matemu, Mwenyekiti wa TACOGA 1984, Sophia Nchimbi,Mshauri wa Wanafunzi ISW na Katibu wa TACOGA 1984, Dk.Andrew Caleb Randa, Mshauri wa Wanafunzi Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) na Naibu Katibu Mkuu wa TACOGA 1984, Mhandisi Saad Hassan
....................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
CHAMA cha Ushauri na Uelekezi kwa Washauri wa
Wanafunzi Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TACOGA 1984)
kimewakutanisha washauri wa wanafunzi kutoka Vyuo vya Elimu
ya Juu, Vyuo vya Kati, Vyuo
vya Ufundi na viongozi wa Serikali za Wanafunzi.
TACOGA 1984
imewakutanisha wadau hao kwa ajili ya kuwawezesha kupata
mafunzo yanayohusu namna bora ya kukuza utendaji katika kuwapa ushauri
wanafunzi wanao walea na kuwaongoza.
Akifungua mafunzo
hayo Juni 21, 2023 kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA),
Mkurugenzi wa TIA Kampasi ya Singida, Dk.James Mrema aliwataka washiriki wa
mafunzo hayo kujikita zaidi katika changamoto zinazo likabili Taifa hasa
suala la malezi ya vijana kutokana na utandawazi.
Dk.Mrema
alisema mmomonyoko
wa maadili kwa vijana ni changamoto katika jamii ya watanzania na unarudisha nyuma maendeleo ya Taifa hivyo ni muhimu
mafunzo hayo yalenge kupanga mbinu za kuwalinda vjana.
“Ifahamike
kuwa kasi ya
kuporomoka kwa maadili inachochewa na ukuaji wa teknolojia ya habari na
mawasiliano ambapo watoto na vijana wanaiga tamaduni na desturi za jamii
zingine zinazo kinzana na mila za mtanzania hivyo hatua za haraka
zisipochukuliwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi,” alisema Mrema.
Dk. Mrema alitoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo wayatumie kama chachu ya kuwawezesha kupata mbinu bora zaidi katika kutatua changamoto za mmomonyoko wa maadili kwa vijana wa taifa la Tanzania.
Alisema
ni matumaini yake kuwa pamoja na kupata mafunzo hayo ya siku tatu, yatakayotolewa
na wataalam tofauti tofauti , pia watapata fursa ya kujadili na kubaini changamoto
mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa jukumu lao la kutoa ushauri kwa
wanafunzi wa vyuo hivyo na kuwa mijadala hiyo itafanyika kwa lengo la kuibua
mbinu bora za kukabiliana na changamoto hizo, ili waweze kuboresha na
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Aidha,
Mrema alitumia nafasi hiyo kutoa pongezi zake za dhati kwa Kamati Tendaji ya
TACOGA 1984, kwa maandalizi mazuri pamoja na kwa
washiriki wote kwa kuitikia wito wa kuhudhuria mafunzo hayo.
Mwenyekitiwa TACOGA1984, Sophia Nchimbi, alisema kazi kubwa wanayoifanya ni kutoa ushauri nasihi kwa wanafunzi na kwa wafanyakazi, kutoa mafunzo kwa Serikali za wanafunzi na kwa sekondari kuhusu mambo mbalimbali ya nasihi na kwa wadau wengine.
Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Matemu alisema chama hicho kina malengo makubwa moja
ya malengo hayo ni kuwajengea uwezo wa washauri wa wanafunzi na wafanyakazi
wote waliopo kwenye ofisi ya ushauri.
Alitaja
lengo lingine kuwa ni kukifanya kuwa ni chama cha watu waliobobea kwa
kutengeneza bodi kama walivyofanya wahasibu, watu wa manunuzi na watu wa rasilimali
watu.
Alisema
kutokana na teknolojia kukua na mambo ya watu kuwa mengi wameona chama hicho
kiwe cha kitaaluma zaidi jambo litakalowasaidia vijana ambao wanakabiliwa na
changamoto nyingi.
Mlezi
wa Wanafunziwa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Mhandisi Saad Hassan ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa TACOGA
1984, alisema chama hicho kipo katika vyuo vikuu vyote vilivyopo Zanzibar na
kuwa wanachama wamekuwa wakishirikiana vizuri katika pande zote za Muungano
yaani Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa
upande wake Mratibu wa madawati ya jinsia wa vyuo vikuu na vyuo vya kati kutoka Wizara ya
Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Gift Msohoya alisema wizara
imeandaa madawati ya jinsia vyuoni kutokana na agizo la Rais Samia Suluhu
Hassan ili kuviwezesha kukabiliana na ukatili wa aina zote na kuwa watendaji
wanayosimamia madawati hayo tayari wapo kazini.
Alisema
hadi sasa vyuo 290 hapa nchini tayari vimekwisha anzisha madawati hayo na lengo
ni vyote viwe nayo.
Mshauri
wa Wanafunzi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni
jijini Dar es Salaam, Ukende Mkumbo, alisema chuo hicho kimekuwa mwanachama hai
wa TACOGA 1984 tangu kianzishwe mwaka 1984.
Alisema
TACOGA 1984 imekuwa msaada mkubwa kwa vyuo kwani imekuwa ikiwanoa washauri wote wa
wanafunzi kwa ngazi zote kwa kuwapa semina, maarifa na mbinu ambazo
zitawasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii na wanafunzi.
“TACOGA 1984 imepewa kazi na Serikali ya kuhakikisha inawanoa vijana hawa kitaaluma watoke kama wataalam wanaoweza kujitosheleza na kujenga nchi na kuwa na mazingira mazuri ya kusomea na kuwasaidia wanaondokana na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kuwafanya wakatishe masomo yao,”alisema Mkumbo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Dk.James Mrema, akifungua mafunzo hayo. Kutoka kushoto ni Makamu Mwenyekiti TACOGA 1984, Augustine Matemu, Mwenyekiti wa TACOGA, Sophia Nchimbi,Mshauri wa Wanafunzi ISW na Katibu wa TACOGA 1984, Dk.Andrew Caleb Randa, Mshauri wa Wanafunzi Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) na Naibu Katibu Mkuu wa TACOGA 1984, Mhandisi Saad Hassan
0 Comments