WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kufanya maboresho ya Sera ya Mifugo na Uvivu ili iweze kuleta tija kwa Taifa.
Amesema hayo leo Jumanne (Mei 02, 2023) alipotembelea maonesho ya wadau wa mifugo na uvuvi yanayoendelea kwenye viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.
Amesema kuwa lengo la kufanya maboresho hayo ni kuhakikisha sekta hiyo inaongeza mchango katika pato la Taifa na uchumi wa mtu mmojammoja. “Sekta ya mifugo na uvuvi ni muhimu sana, ni uchumi na mafanikio ya maisha ya kila siku ya anayejishughulisha na sekta hiyo.”
“Tunajua tuna mafanikio na changamoto, lakini tunataka kuhakikisha Taifa hili linatumia bidhaa zitokanazo na mifugo na uvuvi, suala la masoko ya bidhaa zake ni pana,” amesema.
Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wafugaji nchini wafuge kitaalam. “Tuachane na ufugaji wa kuhamahama, kwani kwa kufanya hivyo tunapunguza ubora wa bidhaa ya mfugo.”
Awali, Waziri wa Mifigo na Uvuvi Abdalah Ulega alimweleza Waziri Mkuu kuwa Kampuni ya ASAS inakusudia kujenga kiwanda cha kutengeneza maziwa ya unga ambacho kitasaidia kumaliza tatizo la maziwa kukosa soko.
Alisema kiwanda hicho kitahitaji maziwa mengi hivyo kitanunua maziwa yote na kuwaondolea wafugaji hasara inayotokana na kukosa soko hasa kipindi cha mvua ambapo uzalishaji wa maziwa unaongezeka.
0 Comments