Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (kulia) akimkabidhi cheti cha ufanyakazi bora, Muhaza Shukuru kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi yaliyofanyika Uwanja wa Liti mjini hapa leo Mei Mosi 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba
ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU)
kushirikiana na vyama vya wafanyakazi kuhakikisha vitendo vya rushwa ya
ngono na unyanyasaji wa kijinsia vinakomeshwa mkoani hapa.
Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema
hayo leo kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kimkoa
katika Uwanja wa Liti mkoani hapa.
"Vitendo vya rushwa ya ngono maeneo ya kazi
na mashuleni vimekuwa vikisikika mara kwa mara nawaomba Takukuru na vyama vya
wafanyakazi hakikisheni muna vikomesha." alisema Serukamba.
Aidha, Serukamba amevisisitiza vyombo vya ulinzi
na usalama kuhakikisha vinaendelea na jitihada za kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inabaki kuwa shwari ndani
ya Mkoa wa Singida.
Alikadhalika Serukamba ameitaka Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii wa NSSF na PSSSF kuhakikisha inawalipa mafao ya wastafu kila mwaka
badala ya kuchelewesha malipo hivyo kuleta hadha kwao ya kufuatilia mafao yao.
Pia Serukamba alisema Serikali inatambua mchango
wa vyama vya wafanyakazi vilivyo chini ya Shirikisho la vyama hivyo (TUCTA) na
jitihada vinavyofanya katika kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi.
Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Singida, Agnes John
akizungumza wakati akitoa taarifa ya chama hicho ameiomba Serikali kuwalipa
mishahara bora ambayo itakidhi mahitaji ya msingi ya binadamu ikiwemo kupewa
ajira yenye staha.
Agnes alisema mshahara bora unawawezesha
wafanyakazi kupata mahitaji yao ya msingi ikiwemo kuweka akiba kwa ajili ya
kusomesha watoto wao na kusaidia katika mambo mengine muhimu ya kimaendeleo.
Alisema kutokana na kulipwa mishahara duni baadhi
ya wafanyakazi wamekuwa na changamoto mbalimbali na kushindwa kuyamudu maisha
yao ya kila siku.
Akizungumzia ajira yenye staha Agnes alisema
kumekuwa na tabia kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa kuwaweka mahabusu
watumishi wa umma pale wanapobainika kukiuka taratibu za utendaji kazi jambo
ambalo ni udhalilishaji mkubwa kwa wafanyakazi hao.
Agnes alitumia nafasi hiyo kuwaomba watumishi
wote mkoani hapa kufanya kazi kwa bidii na kutunza vifaa vilivyoletwa na
Serikali baada ya kukamilisha miradi ya maendeleo kama ujenzi wa vituo vya
aAfya, Hospitali, Shule na Maabara.
Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Singida, Maria Bange
alitaja baadhi ya mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha mwaka 2022/ 2023
kuwa ni waajiri kutoa fursa kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi kutimiza
majukumu yao pasipo kubughudhiwa, ushirikiano mzuri wa vyama vya wafanyakazi na
waajiri hasa wakurugenzi katika halmashauri na kuendelea kuwa na amani katika
nchi yetu kumezidi kuchochea ufanisi kazini maana wafanyakazi hufanya kazi bila
ya hofu.
Bange alitaja mafanikio mengine kuwa ni kupungua
kwa rushwa ya ngono katika harakati za kutafuta ajira, baadhi ya waajiri kutoa
fursa kwa wafanyakazi kujiendeleza kimasomo, watumishi wa Serikali kupandishwa
madaraja kwa waliokuwa wanastahili, watendaji wa kata kupata posho ya mwezi,
waajiri kuitisha vikao vya mabaraza ya wafanyakazi, kupunguzwa kodi katika
mishahara ya watumishi na kuongezwa kwa umri (miaka) ya wategemezi katika
kuhudumiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
Aidha, Bange alitaja changamoto kadhaa kuwa
nyongeza ya mishahara iliyofanyika mwaka jana haikukidhi matarajio ya
wafanyakazi, shirika la bima kutowalipa watumishi waliokata bima ya maisha pindi
bima zao zinapoiva, hivyo kupelekea malalamiko mengi kwa watumishi waliojiunga
na bima hiyo.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni
ucheleweshwaji pensheni kwa wastaafu, madai ya wafanyakazi juu ya fedha za
uhamisho, likizo pamoja na malimbikizo ya mishahara kucheweshwa hadi wengine
kustaafu.
Katika maadhimisho hayo wafanyakazi na waajiri bora walitunukiwa, vyeti, luninga na fedha taslim na vyama vyao vya kazi kama motisha kwao zawadi zilizokabidhiwa na mkuu wa mkoa ambaye alikuwa mgeni rasmi huku maadhimisho hayo yakipambwa na kunogeshwa kwa burudani mbalimbali.
0 Comments