Shirika la umeme Tanzania TANESCO leo kwa mara ya kwanza limeweka historia kwa kusaini mkataba wa kwanza wa kuzalisha umeme kwa wa njia ya jua kwa teknolojia ya “Solar Photo Voltaic” ambapo jumla ya megawati 50 zitazalishwa.
Mradi huu mkubwa kuwahi kutokea wa kuzalisha umeme kwa kutumia jua hapa nchini na katika ukanda wa Afrika mashariki utatekelezwa kwa awamu mbili ambapo katika awamu ya kwanza zitazalishwa megawati 50 Kutoka wilaya ya Kishapu mkoani shinyanga na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika Mei 29, 2023 mjini Dodoma ambapo ilishuhudiwa na waziri wa Nishati Mhe. January MAkamba ambapo aliipongeza TANESCO kwa hatua iliyofikia kupatikana kwa mkandarasi na hatimae kusainiwa kwa mkataba huo ambao utagharinu kiasi Cha shilingi bilioni 275 pindi utakapokamilika .
Mhe. Makamba amesema kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia Nishati jadidifu kwa Sasa WIZARA inaandaa mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa TANESCO inafanya upembuzi yakinifu na kuainisha maeneo ambayo yanafaa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vya Nishati jadidifu."Serikali kupitia WIZARA ya Nishati inakamilisha mpango mkakati wa uwekezaji kwenye maeneo haya kwani kwa sasa yanapewa kipaumbele sana kwenye uzalishaji wa umeme na naiagiza TANESCO itengeneze mwongozo unaoonyesha maeneo yote yanayofaa kwa uwekezaji kwa kutumia Nishati jadidifu" alisema Makamba.
Akizungumza juu ya mradi huo wa kuzalisha umeme kwa njia ya jua mkurugenzi mtendaji wa TANESCO Maharage Chande amesema mradi huo utatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza utazalishwa megawati 50 na awamu ya pili megawati 100 na utatekelezwa na kampuni ya SINOHYDRO CORPORATION kutoka nchini China.
Maharage amesema kusainiwa kwa mkataba huu ni sehemu ya mpango wa mapinduzi katika kuzalisha umeme kutumia vyanzo mbadala ukiacha vile vya maji,na gesi nchini ili kufikia lengo la kuwa na Megawati 5000 kwenye gridi ya taifa ifikapo 2025.
Utekelezaji wa mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mkopo uliotolewa na Shirika la maendeleo la Ufaransa (AFD) unatarajiwa kuanza mwezi juni 2023 ambapo utachukua miezi 14 hadi kukamilika kwake.
Utiaji saini Mkataba huu ulishuhudiwa na Waziri wa Nishati Mhe January Makamba,Naibu waziri wa Nishati Mhe Stephen Byabato, mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule,Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme,Waheshimiwa wabunge viongozi waandamizi wa wizara na menejimenti ya TANESCO waliohudhuria hafla hiyo katika ukumbi wa Morena ulioko Mkoani Dodoma.
Waziri wa Nishati Mheshimiwa January Makamba akishuhudia makabidhiano mara baada ya kusainiwa mkataba wa kuzalisha umeme kwa njia ya jua.
Sehemu ya Wabunge Mkoa wa Shinyanga wakifuatilia jambo wakati wa hafla ya kutia saini mkataba wa kwanza wa kuzalisha umeme kwa njia ya jua.
Waziri wa Nishati Mheshimiwa January Makamba akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba wa kwanza wa kuzalisha umeme kwa njia jua
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Maharage Chande akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dodoma.
0 Comments