Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MKUU wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Edward Mpogolo ametoa maelekezo kwa wafanyabishara katika maeneo ya Kariakoo katika kila meza tatu kunakuwa na chombo cha kuhifadhia taka huku pia wakandarasi nao wakitakiwa kuweka vyombo vikubwa Vya taka katika mitaa.
Mpogolo ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa shughuli za kufanya usafi katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo likiwemo kwanza eneo pia la Soko Kuu la Kariakoo.
Akieleza mbele ya wananchi na wafanyabiashara wa Kariakoo Mpogolo amesema katika kuhakikisha Kariakoo inakuwa safi ni wajibu wa kila mfanyabiashara kuwa sehemu ya kuunga mkono jitihada zinazoendelea ili mazingira kuwa safi wakati wote.
“Kwa wafanyabiashara hakikisheni mnakuwa na chombo cha kuhifadhia taka, na Maelezo haya sio ombi ni lazima, kila baada ya baada ya meza tatu kuwe na chombo cha taka.Kwa wafanyabiashara ambao katika meza zao kutakuwa na taka watatozwa faini na meza itaondolewa kwa wiki moja.
“Na kwa wakandari katika kila mtaa wa Kariakoo kuwe na chombo kikubwa cha kuhifadhi taka.Kukiwa na vyombo vikubwa kwa ajili ya kuhifadhia taka maana yake wafanyabishara vyombo vyao vinapokuwa vimejaa watapeleka katika vyombo vikubwa vilivyopo katika mitaa ya Kariakoo.”
Kuhusu mitaro ya maji kuziba katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo,Mpogolo ametoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROAD) kuhakikisha wanaanza kazi ya kusafisha mitaro hiyo ili maji yatiririke.
Kwa upande wa taa za barabarani Mpogolo amesema Wilaya hiyo imejipanga vema na kusisitiza taa za barabarani zitawekwa katika maeneo yote yaliyokusudiwa huku pia akitoa rai kwa wamiliki wa majengo Kariakoo kuhakikisha nao wanafunga taa.
Pia ametoa onyo kwa wamiliki wa majengo yanayoendelea kujengwa Kariakoo kuacha tabia ya kuweka matofali,mchanga na kokoto kwa muda mrefu katika barabara za mtaani.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kariakoo jijini Dar es Salaam Haji Manara amesema siasa za Kariakoo ni usafi wa mazingira pamoja na utulivu kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo, hivyo usafi ndio kipaumbele kwao.
“Mkuu wa Wilaya ya Ilala jitihada zako kuhusu usafi tunaziona lakini pia tumekuwa na vikao vya mara kwa mara kuzungumzia na kuweka mikakati ya usafi.Pia tunajua dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu Usafi kwa Jiji la Dar es Salaam.”
Manara amesema pamoja na usafi unaoendelea lakini bado kuna baadhi ya mitaa uchafu ni changamoto kutokana na mitaro mingi kuziba, pia kuna mitaa ambayo haipitiki kabisa hivyo ametoa ombi kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala kufungua mitaa hiyo,ombi ambalo limekubaliwa.


.jpeg)

0 Comments