Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa taarifa binafsi nchini ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia za kidijitali, ikisisitiza kuwa faragha ya wananchi ni msingi wa kujenga uchumi wa kidijitali unaoaminika, salama na jumuishi kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Msisitizo huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi lenye kaulimbiu isemayo, "Faragha ya Taarifa ni Nguzo; Kupata Mustakabali Jumuishi wa Kidijitali Kuelekea Dira 2050." Kongamano hilo limewakutanisha wadau kutoka serikalini, sekta binafsi, wataalamu wa TEHAMA na sheria kujadili namna ya kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Mkama, alisema taarifa binafsi ni nyenzo muhimu inayomtambulisha mtu na hivyo zinapaswa kulindwa kwa umakini ili kulinda haki, utu na usalama wa wananchi pamoja na kujenga mazingira rafiki kwa wawekezaji katika uchumi wa kidijitali.
Alisema Serikali ilianzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) mwaka 2022 ili kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha taasisi zote zinazokusanya au kuchakata taarifa za wananchi zinafuata sheria na viwango vinavyotakiwa.
"Uchumi wa kidijitali hauwezi kujengwa kwa teknolojia pekee. Unahitaji uaminifu na usalama wa taarifa zinazochakatwa katika mifumo mbalimbali ya kidijitali. Kadiri huduma za Serikali na sekta binafsi zinavyozidi kuhamia kidijitali, ndivyo ulazima wa kulinda taarifa za wananchi unavyoongezeka," alisema Dkt. Mkama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia, alisema kongamano hilo ni la kwanza kufanyika tangu kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi mwaka 2022 na linatoa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha utekelezaji wa sheria hiyo.
Alisema ongezeko la matumizi ya huduma za kidijitali nchini limeongeza kasi ya ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi, hali inayohitaji mifumo madhubuti ya kulinda faragha ya wananchi na kujenga imani katika matumizi ya teknolojia.
Dkt. Mkilia alisisitiza kuwa faragha ya taarifa binafsi si kikwazo kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali, bali ni msingi wa kujenga uaminifu, usalama na ukuaji endelevu wa huduma za kidijitali nchini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Dkt. Adadi Mohammed Rajabu, alisema maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya akili mnemba (AI) na huduma za mtandaoni, yamefungua fursa kubwa za ubunifu na uwekezaji, lakini pia yameongeza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi bila kuathiri maendeleo ya teknolojia.
Alisema Tanzania inalenga kuwa kitovu cha ulinzi wa taarifa binafsi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kimataifa kwa kuhakikisha maendeleo ya kidijitali yanaenda sambamba na heshima ya utu wa binadamu, uwajibikaji na usalama wa taarifa.
Kongamano hilo la siku tatu litakalomalizika Julai 1, 2026 linatarajiwa kuibua mapendekezo, suluhisho na mikakati mipya ya kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi nchini, huku likitoa fursa kwa wadau wa sekta ya TEHAMA, sheria na sekta binafsi kubadilishana uzoefu kuhusu mustakabali wa uchumi wa kidijitali Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi, lenye kaulimbiu isemayo, "Faragha ya Taarifa ni Nguzo; Kupata Mustakabali Jumuishi wa Kidijitali Kuelekea Dira 2050," lililofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tume hiyo, Dkt. Adadi Mohammed Rajabu akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kwanza la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi, lenye kaulimbiu isemayo, "Faragha ya Taarifa ni Nguzo; Kupata Mustakabali Jumuishi wa Kidijitali Kuelekea Dira 2050," lililofanyika leo jijini Dar es Salaam.

































0 Comments