Hafla ya kutiliana saini ya pande hizo mbili imefanyika juzi jijini Dar es Salaam, ambapo Jumuiya ya Wanafunzi wanaosomea masomo ya Ukaguzi wa Ndani UDSM IAA iliwakilishwa na Rais wa Jumuiya hiyo, Bi. Daines Mbao huku Taasisi ya IIA ikiwakilishwa na Rais wake, Dk. Zelia Njeza.
Akizungumza katika hafla hiyo, iliyofanyika sambamba na utambulisho wa Maadhimisho ya Mwezi wa Wakaguzi wa Ndani, yaani Mwezi Mei wa kila mwaka, Rais wa IIA, Dk. Njeza alisema makubaliano hayo yatasaidia kuhamasisha vijana wengi kujitokeza na kujiunga na masomo ya ukaguzi wa ndani tangu wawapo vyuoni.
Alibainisha kuwa IIA pamoja na IAA zitatumia Mwezi huu wa wakaguzu wa ndani kukuza na kuchochea vipaji vipya vya wakaguzi wa ndani kuanzia ngazi za elimu ya vyuo vikuu, kuwajengea uwezo zaidi na hamasa kusomea masomo hayo ili kupata wataalamu wengi zaidi wa fani hiyo hapo baadaye.
Alisema viongozi na wataalamu watazunguka sehemu mbalimbali kutoa elimu kupitia vyombo vya habari na baadhi ya vyuo vikuu lengo likiwa ni kuchochea vijana shuleni kujiunga na fani hiyo ambayo inaumuhimu mkubwa kwenye maeneleo ya taasisi na taifa kwa ujumla.
"Tutawaelezea hasa wanafunzi vyuoni umuhimu wa fani ya ukaguzi wa ndani na namna gani wanaweza kufikia kuwa wakaguzi endapo watavutiwa na fani hiyo. Lakini pia sisi kama wakaguzi wa ndani tunamiongozo mbalimbali ambayo hutumika tunapokuwa tukitekeleza majukumu yetu.
"Mwezi huu wa tano ni mwezi wa wakaguzi wa ndani, nasi kama wakaguzi wa ndani wa Tanzania tunajumuika na wakaguzi wenzetu ulimwenguni kusherehekea mwezi huu, Tunasherekea kwa namna mbalimbali ikiwemo kuweza kutambua mchango wa wakaguzi wa ndani kwa jamii, kwa taasisi na kwa taifa kwa ujumla."
Aidha pamoja na mambo mengine watatumia muda huo kutafakari kazi zetu huku tukiangalia mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza katika mazingira ambayo tunafanyia kazi, licha ya kutambua kuwa kuna changamoto nyingi katika mazingira tunayofanyia kazi zetu huu ni muda muafaka wa kutoa elimu kwa wadau wetu.
Alibainisha kuwa mwongozo mpya wa shughuli za ukaguzi wa ndani uliopitishwa kutumika duniani kote utaanza kutumika Januari mwakani ili kupata viwango sawa vya ukaguzi maeneo yote, hivyo watatumia mwezi huu Mei kutoa elimu kwa wadau wao na wana tasnia juu ya kanuni mpya na namna ya kuzitumia ili kujiweka tayari zaidi na mabadiliko hayo.
Alisema viwango hivi ni vya kisasa zaidi na vinaendana na maendeleo ya kiteknolojia jambo ambalolinaweza kuchangia kuimarika na kuleta usawa katika shughuli za ukaguzi wa mahesabu ya ndani, "na tunaamini viwango hivi vitachochea shughuli za ukaguzi na kuleta mafanikio zaidi ya fani nzima ya ukaguzi," alisisitiza Rais huyo wa Taasisi ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani nchini.
Tunajikita pia kutoa mafunzo kuelezea hasa shughuli zetu na umuhimu wake kwa jamii. "Sisi kama taasisi ya Wakaguzi wa ndani wa Tanzania tunajivunia kwamba tumefika sehemu ambapo kazi za wakaguzi wa ndani zinatambulika, japo si kwa kiwango kikubwa lakini tunaamini hatua kwa hatua tunaweza kufika mbali zaidi," alisema Dk. Njeza.
0 Comments