Tanzania inaendelea kuimarisha na kuongeza matumizi ya gesi asilia katika uzalishaji wa nishati ya umeme nchini, hatua inayolenga kuiwezesha kufikia lengo la kuzalisha megawati 8,000 za umeme ifikapo mwaka 2030. Katika mpango huo, gesi asilia ni miongoni mwa vyanzo muhimu vitakavyotumika kuimarisha uzalishaji wa umeme wa uhakika na wa kutosha nchini.Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratus Ndejembi, katika Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (World Bank – IMF Spring Meetings 2026) inayoendelea jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Akizungumza katika mjadala kuhusu uzalishaji wa umeme kupitia gesi asilia uliofanyika chini ya mada isemayo “Gas in Sub-Saharan Africa’s Energy Sector”, Waziri Ndejembi amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoweka kipaumbele kikubwa katika kutumia gesi asilia kama chanzo cha kuzalisha umeme.
Ameeleza kuwa hadi sasa, Tanzania inazalisha zaidi ya megawati 1,200 za umeme kupitia gesi asilia, ambazo tayari zimeunganishwa katika Gridi ya Taifa, hatua inayochangia kuimarika kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
Aidha, Waziri Ndejembi amebainisha kuwa serikali inaendelea kuimarisha uzalishaji wa gesi asilia, ambapo kazi ya uchimbaji wa visima vipya vitatu katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara inaendelea. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa gesi na hivyo kuimarisha zaidi uzalishaji wa nishati nchini.
Pia, amesisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya nishati, hususani katika eneo la matumizi ya gesi asilia, ambalo lina fursa kubwa za kiuchumi na maendeleo ya taifa.
Katika mkutano huo, Benki ya Dunia imezitaka nchi za Afrika kuendelea kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia, huku Tanzania ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua muhimu katika matumizi ya nishati hiyo.
Katika Mkutano huo, Waziri Ndejembi ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio pamoja na wataalam kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

0 Comments