.jpeg)
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imewahimiza Watanzania kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa duni na zisizo salama, ikisisitiza kuwa ulinzi wa afya ya jamii ni jukumu la kila mwananchi.
Hayo ameyasema Meneja wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa TMDA, Gaudensia Simwanza, alipokuwa akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la TMDA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam.
Simwanza amesema dawa duni na zisizosajiliwa mara nyingi huingizwa nchini kwa njia zisizo rasmi, hivyo wananchi wanapaswa kuwa macho na kutoa taarifa mara wanapobaini bidhaa zinazotiliwa shaka badala ya kuzifumbia macho.
Ameeleza kuwa matumizi ya dawa duni yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya watumiaji na kuhatarisha maisha ya wananchi, jambo linaloweza kuathiri nguvu kazi na maendeleo ya taifa.
Aidha, amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kukagua tarehe za mwisho wa matumizi wa dawa kabla ya kuzinunua au kuzitumia. Amesema endapo watabaini dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi au zinazoshukiwa kuwa duni, wanapaswa kutoa taarifa TMDA ili zichukuliwe hatua za kuziondoa sokoni.Gaudensia amesisitiza kuwa dawa duni hazina nafasi katika soko la Tanzania, akibainisha kuwa mafanikio ya kuzuia bidhaa hizo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya TMDA na wananchi katika kulinda afya ya jamii.

0 Comments