About Me

header ads

Benki ya Absa Tanzania yaongeza kiwango cha mkopo binafsi na muda wa marejesho kuwawezesha wafanyakazi wa sekta binafsi na ya umma.

Benki ya Absa Tanzania imetangaza maboresho katika bidhaa yake ya Mkopo Binafsi Usio na Dhamana kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na Umma wanaopokea mishahara, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa mikopo nafuu na yenye masharti nafuu zaidi ikiwa ni sehemu ya dhamira ya benki hiyo ya kuiwezesha Africa ya Kesho, pamoja, hatua Moja baada ya nyingine.

Chini ya maboresho hayo mapya, wafanyakazi wa sekta binafsi na umma sasa wanaweza kupata mikopo hadi shilingi milioni 200 za Kitanzania, kutoka kiwango cha awali cha shilingi milioni 150. Aidha, muda wa marejesho umeongezwa hadi miezi 96 (sawa na miaka 8), huku mkopo huo ukiendelea kutolewa bila hitaji la dhamana yoyote.

Huduma hii inawahusu wateja waliopo tayari benki (ETB) pamoja na wateja wapya (NTB), kwa kuzingatia taratibu za kawaida za tathmini ya uwezo wa mkopo.

Maboresho haya yanafuatia hatua kama hiyo iliyotekelezwa awali kwa wafanyakazi wa sekta ya umma, ambapo Absa iliongeza kiwango cha mkopo hadi shilingi milioni 200, kuongeza muda wa marejesho hadi miaka 10, na kupunguza muda wa kusubiri kuongeza mkopo (top-up) kutoka miezi 6 hadi miezi 3.

Hatua hizi kwa pamoja zinaonyesha dhamira endelevu ya Absa kusaidia wateja wanaopokea mishahara katika sekta mbalimbali katika hatua muhimu za maisha yao ya kifedha.

Akizungumza wakati wa kutangaza maboresho hayo, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Ndabu Swere, alisema hatua hiyo imejengwa katika uelewa wa kina wa safari za maisha ya wateja. “Katika Absa, tunaelewa kuwa maisha ya kila mteja ni simulizi, yenye sura tofauti na nyakati muhimu. Iwe uko sekta ya umma au binafsi, jukumu letu ni kuwawezesha wateja kusonga mbele kwa kujiamini. Kwa kuboresha mikopo yetu binafsi isiyo na dhamana, tunawawezesha kusema NDIO kwa maendeleo – kwa sababu stori yao ni ya thamani sana,” alisema Bi. Ndabu.

Bi. Ndabu alisisitiza umuhimu wa unafuu na unyumbufu wa kifedha katika hatua mbalimbali za maisha. “Kuongezwa kwa muda wa marejesho na kiwango cha mkopo kunawapa wateja nafasi ya kusawazisha majukumu ya leo na malengo ya kesho. Kuanzia kuanzisha biashara, kuboresha makazi, kuwekeza katika elimu, kugharamia matibabu hadi kuunganisha madeni, bidhaa hii inawawezesha wateja kujisogeza mbele bila shinikizo lisilo la lazima la kifedha,” aliongeza.

Alibainisha pia kuwa wateja waliopo wanaokidhi vigezo wanaweza kuomba nyongeza ya mkopo au kufanya marekebisho ya mkopo (refinancing), kwa mujibu wa sera za ndani za benki na idhini ya tathmini ya mkopo.

Maboresho haya yanaungwa mkono na kampeni ya wateja ijulikanayo kama “Jisogeze na Mkopo wa hadi TZS 200m”, inayowahamasisha wateja kusonga mbele kwa ujasiri katika safari zao za kifedha.

Wateja wanaweza kuomba mkopo huo kwa kutembelea tawi lolote la Absa, kuzungumza na Afisa Mahusiano au kuwasiliana na vituo vya huduma kwa wateja vya benki hiyo.

Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa Benkiya  Absa Tanzania, Bi. Ndabu Swere (katikati), akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Jisogeze na Mkopo wa hadi TZS 200m”, inayolenga wafanyakazi wa sekta binafsi na umma,  jijini Dar es Salaam leo. Pichani  kushoto ni Bw. Aron Luhanga, Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano  na kulia ni Bw. Heristraton Genesis, Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi.
Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi wa Benki ya  Absa Tanzania, Bw. Heristraton Genesis (kulia), akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi  wa kampeni ya “Jisogeze na Mkopo wa hadi TZS 200m”, inayolenga wafanyakazi wa sekta binafsi na umma,  jijini Dar es Salaam leo. Wengine kutoka kushoto ni Bw. Aron Luhanga, Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano na Bi. Ndabu Swere, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi kutoka benki hiyo.

Post a Comment

0 Comments