About Me

header ads

WIZARA YA ARDHI YAZINDUA MPANGO MAALUM KUINUA WANAWAKE KUPITIA SAMIA ARDHI KLINIKII

 

Na.Mwandishi Wetu-Dodoma

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha  kliniki maalum iitwayo Samia Ardhi Kliniki nchi nzima kwa lengo la kuongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi, ambapo kwa sasa ni asilimia 28 tu.

Hatua hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha huduma za ardhi zinatolewa kwa wananchi kwa kuzingatia misingi ya usawa wa kijinsia.

Akizungumza leo Machi 2,2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Mhandisi Anthony Sanga, amesema mpango huo utaendeshwa nchi nzima na unatarajiwa kuhitimishwa Machi 7 mwaka huu, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Mhandisi Sanga amesema kuwa  lengo kuu la Samia Ardhi Kliniki ni kuongeza asilimia ya umiliki wa ardhi kwa wanawake nchini kupitia utoaji wa elimu, hati za umiliki na utatuzi wa migogoro ya ardhi.

 "Takwimu zinaonesha kuwa ni takriban asilimia 28 pekee ya wanawake nchini wanamiliki ardhi, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha ushiriki wao katika masuala ya umilikishaji."amesema Mhandisi Sanga

Mhandisi Sanga amefafanua kuwa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 iliweka msingi wa usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi kati ya wanaume na wanawake. Hata hivyo, amesema changamoto zilijitokeza katika utekelezaji, hasa kwenye masuala ya mirathi na urithi ambapo mila na desturi zilichangia kuwabagua wanawake.

“Tamko la sera ya mwaka 1995 lilielekeza kuzingatia mila na desturi, lakini katika sera mpya iliyozinduliwa mwaka 2025 na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, haki ya umiliki wa ardhi kwa wote—wanaume na wanawake imewekewa usawa bayana,” amesema Mhandisi Sanga

Aidha amesisitiza kuwa katika sera hiyo mpya, masuala ya urithi na mirathi yameainishwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, hivyo kuweka mazingira rafiki kwa wanawake kumiliki na kurithi ardhi bila ubaguzi.

"Kupitia Ardhi kliniki hiyo maalum, wanawake watapatiwa hati za umiliki wa ardhi, kusaidiwa kutatua migogoro ya ardhi pamoja na kupewa elimu kuhusu haki na taratibu za umiliki wa ardhi."amesema

Amesema mpango huo unalenga kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanawake katika sekta ya ardhi zinatatuliwa kwa wakati, huku ukichochea ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo amewataka kuwa watulivu wakati zoezi hilo likiendelea ili waweze kuhudumiwa kikamilivu na kwa weledi.

Kwa upande wake, Mthamini Mkuu wa Serikali wa Wizara hiyo, Bi. Evelyn Baruti Mugasha, amesema hadi majira ya mchana wanawake zaidi ya 160 walikuwa wamejitokeza kupata hati, huku wengine wakiendelea kujitokeza.

Bi. Mugasha amewataka wanawake wa Mkoa wa Dodoma kutumia fursa ya kliniki hiyo kupata elimu, ushauri na huduma mbalimbali, huku akitoa wito kwa wanaume kutoa ushirikiano ili kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu.

“Kumwezesha mwanamke kumiliki ardhi ni hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wa familia na taifa kwa ujumla,” amesema Bi. Mugasha.

Nao, wanachi wa Mkoa wa Dodoma wamempongeza Rais Samia  kwa kuwapa kipaumbele wanawake katika suala la hati ili kuhakikisha hawabaki nyuma.

Naye mkazi wa Chidachi, Bi. Veronica Hamisi, amesema amefurahi kupata hati aliyokuwa akiifuatilia kwa takribani miaka mitatu ndani ya siku moja.

Kwa upande wake, mkazi wa Miyuji, Getruda Mathias, amesema amehangaika kwa miaka mitano kupata hati, lakini anamshukuru Rais kwa kutoa kipaumbele kwa wanawake kilichomwezesha kupata hati ndani ya saa moja bila usumbufu.

“Nawasihi wanawake wenzangu tujitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa hii ambayo itahitimishwa Machi 7 mwaka huu,” amesema.

Mkazi wa Ilazo, Zena Hamis, pia amemshukuru Rais kwa kuwapa kipaumbele wanawake na kuwasihi wale ambao bado hawajajitokeza kufanya hivyo ili kunufaika na huduma hiyo.

Post a Comment

0 Comments