Waziri Mchengerwa amesema hayo leo Januari 25 2025, wakati alipozungumza na waandishi wa habari akitoa tamko la maadhimisho ya siku ya Ukoma duniani kwenye ofisi za Wizara Jijini Dodoma.
Waziri Mchengerwa amewataka Waganga Wakuu wa Miko ana Wilaya kuhakikisha kaya zote zilizo katika maeneo wanakoibuliwa wagonjwa wapya wa Ukoma zinafuatiliwa na wanakaya wote kufanyiwa uchunguzi na kubaini wenye kuugua Ugonjwa huo na kuwaanzishia matibabu.
“Nichukue fursa hii kuwataka Waganga Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kaya zote zilizo katika maeneo wanakoibuliwa Wagonjwa wapya wa Ukoma zinafuatiliwa na wanakaya wote kufanyiwa uchunguzi na kubaini wote wenye kuugua Ugonjwa wa Ukoma na kuwaanzishia matibabu. Tukifanya hivyo kila Mkoa na Halmashauri na kila mahali tunaweza kutokomeza ugonjwa huu hata kabla ya Mwaka 2030,” amesema Mhe. Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa ameitaka Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wagonjwa wote wanaoibuliwa wanatambuliwa makazi, Kijjji, na Kata anakotoka, ndani ya Wilaya husika au nje ya Mkoa huku akisema iwapo mgonjwa atatokea nje ya Mkoa, ihakikishwe ya kuwa taarifa zake zinapelekwa alikotokea ili kufanya ufuatiliaji na kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa Ukoma na kuwapatia tibakinga kaya husika.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema tangu mwaka 2006, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitangaza Tanzania kuwa tayari imefikia kiwango cha kimataifa cha kutokomeza ugonjwa wa Ukoma cha chini ya mgonjwa mmoja kati ya watu 10,000 ambapo idadi ya wagonjwa wapya wanaogunduliwa nchini inaendelea kupungua kutoka wagonjwa 2,297 mwaka 2015 hadi wagonjwa 1442 mwaka 2025 sawa na punguzo la asilimia 37.
Waziri Mchengerwa amewashukuru watoa huduma katika vituo vya huduma za afya nchini kwa juhudi za kuboresha afya za wananchi na kuhakikisha ugonjwa wa Ukoma unapungua kasi ya kusambaa nchini. Huku akiwapongeza wanahabari kwa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu afya bora na namna ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali ukiwemo Ugonjwa wa Ukoma.
“Mikoa na halmashauri inabidi mhakikishe kila mgonjwa anayeibuliwa anatambulika anakotoka na taarifa zake zifanyiwe kazi ili kukata mnyororo wa maambukizi, niwashukuru watoa huduma kwa juhudi zenu za kutibia wananchi na wanahabari ambao mnasambaza elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa huu,” amesema Mhe. Mchengerwa


0 Comments