About Me

header ads

Wadau wa Sheria wapongeza ofisi ya Mwandishi Mkuu kwa kuandika sheria timilifu

 

Na: Calvin Gwabara – Dar es salaam.

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bi. Amina Talib Ali, amesema Tume hiyo ni mdau mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) hasa katika kuhakikisha sheria zinaandikwa kwa kuzingatia Haki na Utawala Bora.

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bi. Amina Talib Ali akipokea zawadi kutoka kwa Bw. Philemon Mrosso Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD Bandani hapo.

Hayo ameyasema wakati alipotembelea Banda la OCPD kwenye maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya SabaSaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwl. Nyerere Jijini Dar es salaam.

“Moja ya vitu vya msingi THBUB inatakiwa kuzingatia ni kuhakikisha kuwa Sheria zinazotungwa zinazingatia mikataba ambayo Tanzania imeridhia kuhusiana na haki za binadamu na utawala bora. Kwa minajili hiyo, sisi ni wadau wakubwa wa mchakato mzima wa uandishi wa sheria.” Alieleza Kamishna Ali.

Katika kufafanua ushiriki wa THBUB katika mchakato mzima wa uandishi wa sheria, alieleza kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 130 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kifungu cha 6 cha Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sura ya 391, THBUB ina majukumu ya kutoa mapendekezo kuhusu sheria zilizopo au zinazopendekezwa, kanuni au masharti ya kiutawala kwa madhumuni ya kuhakikisha uzingatiaji wa misingi ya haki za binadamu na utawala bora. Aidha, THBUB pia inahamasisha kuridhiwa au kujiunga na mikataba au makubaliano yanayohusiana na haki za binadamu ikiwa ni Pamoja na kuratibu sheria za Tanzania ziendane na mikataba hiyo na kufuatilia na kutathmini uzingatiaji wa haki za binadamu ndani ya Jamhuri ya Muungano, Serikali au watu wengine.

Aidha Kamishna Ali ameongeza kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo zimeridhia mikataba mingi ya kimataifa inayohusu haki za binadamu na utawala bora hivyo katika utekelezaji wa shughuli zake, lazima ihakikishe haivunji kipengele chochote katika mkataba iliyoiridhia katika nyanja hizo.

“Naielewa sana kazi nzuri na kubwa mnayoifanya katika uandishi wa sheria za nchi, na tunatambua mchango wenu katika kuhakikisha mapendekezo ya kutunga au kurekebisha sheria na sera zinazoletwa kwenu kwa ajili ya kuzifanya kuwa sheria. Hakika mnafanya kazi nzuri ya kuzingatia mambo muhimu ya haki za binadamu na utawala bora zinazingatiwa.” Alieleza Kamishna Ali.

Bw. Philemon Mrosso Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD amemueleza Kamishna makujukumu makuu ya OCPD kuwa ni; kuandika sheria, kufanya urekebu wa sheria, kufanya ufasili wa sheria pamja na nyaraka zote za kisheria zinazowasilishwa Bungeni na masuala mengine yote yanayohusiana na uandishi wa sheria.

Bw. Mrosso alieleza, ili kuwezesha utekelezaji wenye ufanisi wa majukumu ya Ofisi hiyo, wamekuwa wakitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa waandishi wa sheria na mawakili wa serikali kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kufahamu masuala yote ya msingi wakati wa uandishi wa sheria.

Akieleza kuhusu kusitishwa kutumika kwa Toleo la Urekebu wa Sheria la Mwaka 2002 pamoja na matoleo mengine yote yaliyofuata, Bw. Vincent Masalu mwandishi wa sheria kutoka OCPD amewataka wadau wa sheria na nchini kutambua kuwa toleo hilo limesitishwa kutumika rasmi tarehe 1/07/2025 kufuatia tamko rasmi la Mheshimiwa Rais alilolitoa tarehe 24 Aprili 2025 wakati akizindua Toleo la Urekebu wa Sheria la Mwaka 2023.

“Toleo jipya la urekebu la mwaka 2023 lenye jumla ya sheria kuu 446 zilizofanyiwa Urekebu ndilo limeanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai 2023, hivyo kuanza kutumika kwa Toleo jipya la mwaka 2023 kunasitisha matumizi ya matoleo yote ya urekebu ya miaka ya nyuma kabla ya toleo hili jipya la urekebu la mwaka 2023” alifafanua Bw. Masalu.

Aidha, Bw. Masalu alieleza kuwa kwa kutekeleza amri hiyo ya Mheshimiwa Rais, Sheria zote zilizofanyiwa urekebu mwaka 2023 tayari zimewekwa katika tovuti ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nakala mango za sheria hizo zinaendelea kusambazwa katika Wizar ana taasisi zote za umma, lakini pia nakala nyingine za sheria hizi zinasambazwa na kuuzwa kwa wananchi wote.

Bw. Masalu amesema juhudi hizi zote ni katika kuhakikisha kuwa sheria hizi zinawafikia wadau na wananchi ili kurahisisha upatikanaji wake na kupunguza changamoto ya suala zima la kutumia sheria ambazo ni vipandevipande vinavyoleta ugumu katika kufanya rejea na hata upatikanaji haki.

Katika hatua nyingine Bi Mariam Possi, mwandishi wa sheria, aliwasihi wananchi, wadau na umma kwa ujumla kufika katika banda la OCPD ili kuweza kupata elimu kuhusiana na mchakato mzima wa uandishi wa sheria nchini na kupata fursa ya kuona majuzuu ya Toleo la Urekebu wa Sheria la Mwaka 2023 pamoja na kupata nakala ya machapisho mbalimbali yanayotumika na Ofisi yetu katika kutekeleza majukumu haya adhimu kwa mustakabali wan chi yetu.

“Moja kati ya majukumu yetu ni kutoa elimu kwa umma kuhusiana na mchakato wa uandishi wa sheria. Hivyo tumefungua milango yetu kwa kuileta Ofisi yetu karibu na wananchi katika maonesho haya ya kimataifa waweze kuijua na kupata elimu moja kwa moja kutoka kwa waandishi wa sheria ambao usiku na mchana wanafanya kazi kwa weledi na ufanisi ili kuhakikisha sheria zinaitikia kauli mbiu yake ya “Sheria Fasaha kwa Utekelezaji Bora”.” Alisisitiza Bi. Possi.


Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bi. Amina Talib Ali akizungumzia mahusiano ya kiutendaji yaliyopo kati ya Tume na OCPD.

Bw. Philemon Mrosso Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD akitoa maelezo na ufafanuzi kuhusu majukumu ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa Kamishna Ali bandani hapo.

Bi Mariam Possi, mwandishi wa sheria kutoka kwenye Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini akitoa elimu kwa wananchi waliofika kwenye banda la ofisi hiyo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba jijini Dar es saalam.

Bw. Vincent Masalu mwandishi wa sheria kutoka OCPD akiwa ameshikilia moja ya juzuu la Toleo la urekebu wa sheria la mwaka 2023 na kutoa maelezo kwa mwananchi.

Watumishi wa ofisi ya OCPD wakimkabidhi zawadi Afisa Uchunguzi mwandamizi wa Tume ya haki za binadamu na utawala Bora Bwana Pontian Kitorobombo.

Bi. Happyphania Erick akimuonesha mdau wa sheria kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali moja kati ya vitabu vyenye Istilahi za maneno ya Kisheria zilizoandaliwa na OCPD kwenye banda la ofisi hiyo kwenye maonesho ya sabasaba.





Post a Comment

0 Comments