Na Emmanuel Massaka,Tabora
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imepongezwa kwa kazi kubwa ya udhibiti wa dawa nchini sambamba na ujenzi wa makao makuu ya kanda ya TMDA katika Mkoa wa Tabora ambayo ni heshima kubwa ya Mkoa huo.
Pongezi hizo zimetolewa leo Julai 16,2025 na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paulo Chacha alipokuwa akifungua kikao kazi cha wahariri kilichofanyika mjini Tabora ambapo pia ameeleza wamejipanga kuhakikisha hati miliki ya kiwanja inatolewa haraka ili kuruhusu ujenzi wa jengo hilo uanze.
Chacha amesema kwamba Tabora ina umuhimu wa kimkakati kutokana na kupitiwa na reli ya kisasa (SGR) huku akifafanua kuwa maboresho makubwa katika sekta ya afya yamefanyika chini ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan .
Ametaja maboresho hayo ni yamehusisha kuimarisha taasisi kama TMDA na hiyo ni hatua muhimu kwa ustawi wa afya ya jamii ya Watanzania.
Mkuu wa Mkoa huo ametumia nafasi hiyo kuelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la matangazo holela ya dawa za binadamu, hivyo ametoa mwito kwa TMDA kushirikiana na vyombo husika kudhibiti hali hiyo.
“Pia ni vema wafanyabiashara wakaelemishwa kuhusu madhara ya dawa na vifaa tiba bandia na duni ambavyo si salama kwa matumizi ya binadamu.”
Ameongeza baada ya utafiti huo kukamilika, watakuwa katika nafasi nzuri ya kuchukua hatua stahiki kudhibiti tatizo hilo.
Kuhusu kikao cha wahariri amesema lengo la kikao hicho ni kuongeza uelewa wa wahariri kuhusu majukumu ya TMDA na kuonyesha mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.Ametaja baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na usajili wa jumla ya dawa 8,332 katika kipindi hicho, hatua iliyosaidia kupanua upatikanaji wa dawa muhimu kwa wananchi.
0 Comments