Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WANUFAIKA wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) katika Kijiji cha Igenge Kata ya Mbarika, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wameishukuru Serikali kwa kuwainua kiuchumi kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini ambao pamoja na kuwapa ruzuku ya zaidi ya milioni 22 lakini pia imetekeleza miradi mbalimbali.
Wakizungumza wakati walipotembelewa na wajumbe wa kamati ya kitaifa ya uongozi ya Tasaf, wanufaika hao wamesema ruzuku hizo zimeinua uchumi wa familia zao pamoja na kumudu gharama za vifaa vya shule vya watoto wao.
Katibu wa Kikundi cha Mliman City ambacho ni miongoni mwa wanufaika wa Tasaf, Hellena Kazungu amesema katika kikundi chao chenye wanachama 12, walipata ruzuku ya zaidi ya Sh4 milioni ambayo walinunua vifaa vya kutengenezea batiki.
Amesema baada ya kutengeneza na kuuza batiki hizo kila mwananchama alipata faida ya zaidi ya 100,000 lakini pia kupitia kikundi chao na miradi mingine ya Tasaf amefanikiwa kuvuta maji ya bomba nyumbani kwake na kuondokana na changamoto ya kubeba maji kichwani.
Philipo Kapembe ambaye pia ni mnufaika wa Tasaf kijijini hapo amesema kupitia kikundi cha mlimani City amenufaika mambo mengi ikiwemo kusomesha watoto wake lakini pia kuanzisha mradi wa bustani ambao analima mboga mboga na kuziuza.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Robert Manene amesema mpango wa Tasaf kijijini hapo umesaidia kukuza uchumi wa familia na kupungufa ugomvi uliokuwa ukitokana na mahitaji ya chakula kwenye kaya kati ya mme na mke.
Akizungumza baada ya kujionea shuguli za ujasiriamali za kikundi cha Mliman City pamoja na kutembelea shamba la miti la wanufaika wa Tasaf katika kijiji hicho, Mjumbe wa Kamati ya Tasaf, Dk Naftali Ng’ondi amesema lengo la kufika kijijini hapo ni kukagua na kutembelea utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa kuanzisha vikundi vya kuweka akiba pamoja na kuzalisha mali.
“Miradi hii inakuja chini kabisa ngazi ya vijiji, ikitumika vizuri na kwa upana zaidi inaweza kuboresha na kubadilisha maisha ya wananchi,”amesema
Kijiji cha Igenge kina kaya 653 wakazi 4,237 huku walengwa wa tasaf wakiwa 111 baada ya kutambuliwa na kuingia katika mpango wa kunusuru kaya masikini awamu ya tatu na Mkoa mzima wa Mwanza wenye wilaya saba una wanufaika zaidi ya 42,588.
0 Comments