Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Mh.Suleiman Jafo ameishauri bodi mpya ya Wakurugenzi wa Tume ya Ushindani( FCC) kuhakikisha inakutana na kufanya kikao haraka kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali pamoja na kupitia mambo yote yanayotakiwa kupatiwa ufumbuzi kuhusu masuala ya uwekezaji nchini.
Ametoa ushauri huo leo Oktoba 4,2024 Dar es Salaam alipokuwa akizindua bodi hiyo, ambapo amesema bodi hiyo inajukumu la kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika maono yake yakuvutia wawekezaji na kukuza uchumi nchini.
Amefafanua kwamba FCC ni injini ya uwekezaji Nchini,hivyo bodi hiyo mpya itasaidia Wizara ya Viwanda na Biashara katika kuhakikisha Sekta Binafsi inakua kwa kasi nakuleta mchango wa maendeleo pamoja na kuondoa changamoto ya ajira kwa Vijana.
Waziri Jafo amesisitiza sekta binafsi ndio suluhisho la kujibu mahitaji ya ajira kwa Vijana wanaohitimu kila Mwaka ,na jukumu hilo wamepewa umepewa Wizara ya Viwanda na Biashara,hivyo ameiomba FCC ifanye kazi yake kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.
"Nawashauri watendaji wa FCC kufanya kazi kwa kuzingatia mabadiliko ya sheria katika kufanya tathmini ya namna makampuni yanavyoweza kuungana ili kuleta tija katika ushindani kibiashara."
Pia amewataka watendaji wa Tume ya Ushindani kutoa ushirikiano wa dhati kwa Bodi ya Wakurugenzi ili iweze kufanya kazi nakufikia malengo waliyojiwekea,nakwamba bodi hiyo isipofanya kazi zake vizuri inaweza kuiyumbisha Serikali.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa maono ya kuweka mazingira rafiki na tulivu ya ufanyaji biashara.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya FCC Dkt.Aggrey Mlimuka amemhakikishia Waziri Jafo kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa kwa Bodi hiyo.
Amesisitiza kuwa watafanyia kazi yote waliyoelekezwa na Waziri Jafo ma kuongeza bodi hiyo anamatumaini itafanya kazi kwa weledi mkubwa katika kumsaidia Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa lengo kuendelea kuvutiwa wawekezaji nchini.
0 Comments