Viongozi wapya wasimikwa akiwemo Profesa Rwekaza Mukandala
Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT) kimepata Viongozi wapya, watakao kiongoza chuo hicho baada ya mwekezaji wa kwanza kushindwa.
Walioteuliwa kuongoza chuo hicho ni Mkuu wa Chuo, Dkt. Kyung Chul Kam, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Sung Soo Kim na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala.
Akizungumza wakati wa Hafla ya kuwasimika Uongozi huo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho anayeshughulikia masuala ya mipango, Fedha na Utawala, Profesa John Mwita alisema sababu za kuchagua uongozi mpya ni kutokana na uongozi uliokuwepo kushindwa kufanya kazi.
"Shinikizo kubwa ni Serikali kuwa na wasiwasi kuhusu uwezo wa mwekezaji kuendeleza kwenye eneo ambalo lina ekari 150 na tangu chuo kimeanza rasmi 2012.
"Kwa hiyo mwekezaji wa kwanza ikabidi atafute mwekezaji mpya ambaye ni CTS ambayo ni Kampuni kubwa ya Television kule nchini Korea ambao wamekuja kununua chuo na kila kitu," alisema Profesa Mwita.
Alisema Chuo hicho kimesajiliwa rasmi na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kina hadhi ya Chuo Kikuu kinatoa fani za biashara na Uhandisi.
Kwa upande wake aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mukandala ambaye pia amesimikwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, alisema bado kuna changamoto ya kuwa na vyuo vikuu kutosheleza idadi kubwa ya vijana wanaohitaji elimu ya juu.
"Bado tuna changamoto ya kuwa na nafasi za kutosha kwa wanafunzi ambao wanahitaji kusoma vyuo vikuu, kwa hiyo hawa wenzetu kutoka Korea Kusini wamejitolea kuanzisha chuo nchini.
"Mwekezaji wa kwanza hakuweza kuendesha vizuri kwa hiyo amepatikana mwingine. lengo ni kuhakikisha chuo kinakuwa na misingi mizuri, miundombinu ya kutosha, vifaa pamoja na karakana ya uhandisi ili waweze kuchukua wanafunzi wengi katika fani mbalimbali," alisema na kuongeza kuwa:
"Kwa sasa tuna fani chache lakini kutakuwa na mabadiliko hivyo nawakaribisha watu waje wajiunge na chuo hiki,".
0 Comments