About Me

header ads

WAUGUZI SUA WAASWA KUKIISHI KIAPO CHAO CHA KAZI WAKATI WA UTOAJI WA HUDUMA KWA JAMII



Na: Calvin Gwabara – Morogoro.

Wauguzi katika Hospitali za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kuzingatia viapo vyao kwa kutoa huduma bora kulingana na maadili ya kazi yao kwakuwa umuhimu wa kazi hiyo ndio unaowatofautisha na kazi zingine ambazo hazitoi viapo kwa taaluma zao.

Kauli hiyo imetolewa na Daktari Mkazi wa hospitali za SUA Dkt. Omary Kasuwi wakati akihitimisha wiki ya Wauguzi iliyofanywa na Wauguzi wa hospitali hiyo wakiungana na wauguzi wengine duniani ambayo ilihusisha wao kufanya kazi mbalimbali kwa jamii ikiwemo kufanya vipimo na ushauri, Kufanya usafi na kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa hospitalini hapo.

“Ndugu zangu nyinyi lazima mtambue kuwa sio kila taaluma wanapewa viapo vya kazi, kiapo ni kitu kikubwa sana kwa mtu au taaluma ndio maana unaweza kuona ni taaluma chache sana zinazotoa viapo, Kiapo kina maana kubwa sana kiroho na kimaadili katika utoaji wa huduma hivyo pamoja na changamoto mbalimbali mnazokabiliana nazo lakini niwakumbushe kuviishi viapo vyenu maana Mungu anaona kazi kubwa mnayoifanya kwa watu wake” alifafanua Dkt. Kasuwi.

Amesema kuna jitihada kubwa zinafanywa kupitia hospitali hiyo na Menejiment ya SUA katika kupunguza baadhi ya changamoto walizoainisha hivyo amewataka kuendelea kufanya kazi kwa moyo kuhudumia jamii na pindi fedha zitakapopatikana changamoto hizo ikiwemo uchache wao na mahitaji mengine yatatatuliwa ili kuzidi kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Kwa upande wake Matroni wa hospitali za SUA Bi. Akaanashe Makere amempongeza Menajimenti ya SUA kupitia kwa Dkt. Kasuwi kwa namana anavyopigania Kurugenzi ya afya Chuoni hapo na fani ya uuguzi kwa pamoja kwa kuweka kipaumbele zaidi kuona huduma bora zinatolewa kwa wanaohitaji taaluma yao hasa katika kupigania upatikanaji wa madawa na vifaa tiba huku akihakikisha utoaji huduma unakuwa rafiki kwa wafanyakazi wote.

“Umekuwa ukijitolea muda wako mwingi sana kutupatia elimu sehemu za kazi ili kuboresha utendaji wetu hivyo tunakuahidi kuwa tutazidi kufanyia kazi yale yote unayotuelekeza na tutakuwa bora zaidi lakini niwatake pia wauguzi wenzangu kujiendeleza katika nyanja mbalimbali pale fursa inapopatikana na tutumie mitandao kujiendeleza na masomo tunayopata mara kwa mara wakati wa vikao vya kila siku asubuhi kwaajili ya kupata alama za kuhuisha leseni zetu” Alieleza Matroni Makere.

Akisoma risala ya wauguzi kwa niaba ya wauguzi wenzake Bi. Joraphina Manyelezi amesema siku ya wauguzi duniani huadhimishwa tarehe 12 mwenzi mei kila mwaka kwa lengo la kumuenzi muasisi wa taaluma ya wauguzi dunaiani aliyefahamika kwa jina la Florence Nightingale aliyefanya kazi kwenye mazingira magumu vitani akiwahudumia majeruhi usiku na mchana kwa kujitolea na baadae huduma hii ya uuguzi iliendelea kuboreshwa katika mazingira ya utoaji huduma na pia uandaaji wa mitaala ya kufundishia.

“ Lengo la maadhimisho haya ni kukumbushana kuhusu taaluma, wajibu wa kazi ya uuguzi na maadili yake na katika kutekeleza lengo la maadhimisho haya wauguzi wa SUA tulijumuika kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii kama vile kupima shinikizo la damu, Sukari, Maambukizi ya VVU kwa hiari pamoja na elimu ya afya ambapo jumla ya watu 62 walipimwa katika kipindi cha wiki moja, lakini pia tumefanya shughuli za kuwafariji wagonjwa kwa kuwapa zawaid mbalimbali na kuendesha zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo ya hospitali ya Chuo” alisema Bi. Munyerezi.

Nae mwenyekitiwa Chama cha wauguzi Tanzania Tawi la SUA Bwana Priscus Uisso Nassoro amewapongeza wauguzi wote kwa kujitoea kwa hali na mali katika kufanikisha maadhimisho hayo Chuoni hapo bila kujali uchache wao na kushukuru Uongozi wa hospitali kwa ushirikiano kuwezesha wauguzi hao kupewa ruhusa kuadhimisha siku hiyo muhimu kwao.

“Kwakweli kupitia shughuli za upimaji tulizozifanya kwanza tushukuru jamii kujitokeza katika kupata vipimo na ushauri lakini tuseme tuu kuwa jamii yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiafya hivyo tunaahidi kuendelea kushirikiana na Chuo na Serikali yetu katika kupunguza changamoto hizo kwa kufanya kazi kwa weledi lakini pia mwakani tunatarajia kufanya vizuri zaidi kwa kuanza maandalizi mapema” alifafanua bwana Nassoro.

Katika kuhitimisha shughuli hiyo wametoa zawadi pia kwa Daktari mkazi wa hospitali ambaye nae amewapa zawadi kwa kazi yao nzuri lakini pia wamekula kiapo cha uaminifu na utiifu katika kazi sambamba na kauli mbiu yao ya mwaka huu isemayo “Wauguzi sauti inayoongoza, wekeza katika uuguzi,heshima haki linda Afya”.Daktari Mkazi wa Hospoitali za SUA Dkt. Omary Kasuwi akitoa neno kwa wauguzi wakati akihitimisha Maadhimisho ya wiki ya Wauguzi duniani Hospitalini hapo.Matroni wa Hospitali za SUA Bi. Akaanashe Makere akitoa neno la ukaribisho kwa Mkgeni rasmi wakati wa kufunga Maadhimisho ya wiki ya Wauguzi duniani katika hospitali hiyo.Bi. Joraphina Manyelezi (Kushoto) akisoma risala ya wauguzi kwa niaba ya wauguzi wenzake, kulia kushoto kwake ni Bi Agatha Aldof.Mwenyekitiwa Chama cha wauguzi Tanzania Tawi la SUA Bwana Priscus Uisso Nassoro akitoa salamu za TANNA – SUA kwa mgeni rasmi.

Picha ya Pamoja ya baadhi ya wauguzi wa Hospitali za SUA pamoja na Daktari mkazi wa Hospitali za SUA Dkt. Omary Kasuwi walioshiriki kwenye maadhimisho hayo kwa niaba ya wenzao ambao walikuwa kwenye majukumu mengine ya kazi.
Dkt. Omary Kasuwi akipokea zawadi kutoka kwa Wauguzi kama sehemu ya kutambua mchango wake katika kufanikisha wauguzi kutimiza majukumu yao na kuishi viapo vyao.

Daktari Mkazi wa Hospitali za SUA Dkt. Omary Kasuwi akimkabidhi keki matroni wa hospitali za sua Bi. Akaanashe Makere kwa niaba ya wauguzi wengine kama sehemu ya kutambua mchango wao katika kutoa huduma bora kwa jamii.


Wauguzi wakila kipo cha maadili ya kazi yao mbele ya Dkt. Mkazi wa Hospitali za SUA Dkt. Omary Kasuwi.

Post a Comment

0 Comments