About Me

header ads

“DKT. BITEKO AZINDUA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA MKOANI NJOMBE”.

 



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishari Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua kampeni ya Msaada wa Kisheria – Mama Samia Legal Aid Campaign Mkoani Njombe; ambayo mpaka sasa imefika katika Halmashauri 42, kata 452 na Vijiji 1,348 kote Nchini.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo leo tarehe 26 Mei -2024; Dkt Biteko ameishukuru na kuipongeza Wizara ya Katiba na Sheria chini ya Waziri Mhe. Pindi Chana kwa kubuni, kuanzisha na kuipa hadhi kubwa kampeni hiyo.


Amesema amefurahi kusikia kupitia kampeni hiyo zaidi ya watu 415,597 wamesikilizwa, kati ya hao Wanaume ni 216,000  na Wanawake ni 199,000 hali inayoonesha kwamba Wanaume wengi wameendelea kujitokeza kwa wingi kupatiwa msaada wa Kisheria.


Ameeleza kuwa Serikali iliamua kuja na kampeni hiyo kwa lengo la  kuwasaidia Wananchi hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za kisheria katika utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala pamoja na kuongeza uwajibikaji wa watendaji na kuimarisha umoja na utengamano miongoni mwa Jamii.


“Baadhi ya maeneo Wananchi wamekiri kuwa migogoro inayodumu kwa muda mrefu, imeweza kutatuliwa ndani ya muda mfupi kupitia kampeni hizi tunazozifanya tena kwa amani,  upendo na kuacha utulivu miongoni mwetu” ameeleza Dkt. Biteko


Ametoa wito kwa Wananchi hasa wale ambao wanadhani hawana uwezo kumudu gharama za Mawakili kutumia fursa hiyo kukutana na Wataalam waliopo kwenye kampeni hiyo ili waweze kusikilizwa, kupatiwa ushauri na hatimaye kumaliza migogoro yao.


Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pindi Chana amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa haki huku akikumbusha kuwa Mhe. Rais ameunda tume ya haki jinai ambayo ilizunguka Tanzania nzima kuja na maoni ya jinsi ya kuboresha masuala ya Utawala wa Sheria.


“Tunaposema Msaada wa kisheria, mtoa msaada nambari moja ni Rais Dkt. Samia, sote ni mashuhuda anapokwenda kwenye ziara anasimama kuwasikiliza Wananchi; Mhe. Rais Mwenyewe siku zote amekuwa mfano na sasa hivi ametuelekeza muende kwa Watanzania mkawasikilize wana changamoto gani na muwaelekeze namna ya kutatua masuala yote ya kisheria’’ ameongeza  Waziri Pindi Chana.






Post a Comment

0 Comments