About Me

header ads

GEF KUPITIA UNDP YATOA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 4 KWA CSOs 44 NCHINI KUTEKELEZA MIRADI NGAZI YA JAMII

 


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.

Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia Programu ya Ruzuku ndogo inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limesaini makubaliano ya kutoa sh 4.04 bilioni kwa mashirika yasiyo ya kiserikali 44 nchini ili kutekeleza miradi ya Uhifadhi wa Mazingira, Misitu, kuendeleza ufugaji nyuki, kutunza vyanzo vya Maji na uwezeshaji Jamii kiuchumi.

Utiaji saini wa Makubaliano hayo umefanyika leo April 4, 2024 katika Makao Makuu ya Jengo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania na kuongozwa na Mwakilishi Mkaazi wa UNDP, Bw. Shigeki Komatsubara.

Miongoni mwa mashirika yaliyosaini mkataba wa kupatiwa fedha hizo ni Shirika la Connecting Youth Connecting Tanzania (CYCT) ambalo limekuwa likihamasisha uhifadhi wa mazingira, Misitu na Mabadiliko ya tabia nchi kuhusisha vijana, Wanawake na Wanafunzi na Kundi la watu Maalum

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Komatsubara amesema kuwa mashirika zaidi ya 400 yalituma maombi kuomba fedha za kutekeleza miradi midogo midogo nchini Tanzania bara na Zanzibar lakini ni mashirika 44 tu ndio yamefanikiwa.

“Hongereni sana leo kuwa miongoni mwa mashirika na asasi ambazo zimepata fursa kutekeleza miradi midogo Tanzania.

Bw. Komatsubara amesema anaimani kubwa mashirika ambayo yanapewa fedha hizo yatakwenda kutekeleza vyema miradi ambayo itagusa jamii hasa wanawake, vijana, Walemavu na Jamii za pembezoni.

“Tunatarajia miradi yetu itakwenda kuchochea maendeleo katika jamii ikiwepo pia kukabiliana na vichocheo vya uharibifu wa mazingira” amesema.

Naye Mwakilishi kwa niaba ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Bi. Lilian Lukambuzi akizungumza katika hafla hiyo alitaka mashirika yaliyopewa fedha hizo kuzitumia kama ilivyokusudia.

Amesema serikali itafuatilia miradi ambayo inakwenda kutekelezwa ili kuhakikisha inakuwa na tija.

Awali, mratibu wa programu ya ruzuku ndogo za GEF nchini, Bw. Faustine Ninga amesema haikuwa kazi rahisi kupitisha mashirika hayo machache kupata ruzuku kutokana na uhitaji mkubwa kutoka katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kamati ya Uendeshaji ya programu hiyo ya Ruzuku Ndogo za GEF ambayo inaundwa na wataalam kutoka sekta mbalimbali na taasis zisizo za Kiserikali kwa kushirikia na UNDP ilifanya kazi kubwa ya kuchambua maandiko ya miradi zaidi ya 400.

Hata hivyo, amesema kutokana na uhitaji kuwa mkubwa ni mashirika 44 tu ndio yalipitishwa, ijapokuwa mashirika mengine yalikuwa na madokezo mazuri ya miradi.

Hata hivyo ameyataka mashirika haya kufuata kanuni na taratibu za nchi na miongozi ya uendeshaji wa taasisi zisizo za kiserikali katika utekelezaji wa miradi yao ili miradi iwe na matokeo mazuri.

Amesema kamati ya ufuatiliaji miradi hiyo itakagua na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ili kuhakikisha kuwa jamii zinanufaika.

Wakizungumza baada ya kusaini mikataba baadhi ya watendaji wa mashirika hayo walipongeza UNDP kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi midogo katika jamii.
Mratibu wa Shirika la CYCT, Bw. Mensieur Elly amesema hii ni mara ya kwanza shirika hilo kupata fedha kutoka kwa wahisani hao.

“Tunatarajia kushirikiana na wadau mbalimbali ambao wamekuwa mstari wa mbele kutunza Ikolojia ya mlima Kilimanjaro kupitia kampeni ya “Go green, serve Nature “ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Siha, Mkurugenzi Siha, TFS West na North Kilimanjaro, Afisa mipango na maendeleo jamii, Afisa elimu, mwenyekiti wa Halmashauri, afisa Tarafa, afisa Mtendaji, madiwani na vikundi vya vijana na wanawake West Kilimanjaro katika kutekeleza na kupata matokeo chanya na yanayoshikika.

Nae mratibu miradi wa Shirika la WODSTA, Bi. Clara Chuwa amesema wanakwenda kutekeleza mradi kwa ajili kuwezesha kutunza mazingira na matumizi endelevu ya msitu na chanzo cha maji kijiji Cha lemanda, Kata ya Oldonyosambu, Wilaya ya Arumeru.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la SECCA, Bw. Esaya Yusufu amesema wanakwenda kutekeleza mradi wa upandaji miti na kuchimba kisima katika eneo la ikolojia ya Serengeti.

Mfuko wa mazingira Duniani (GEF) ulianzishwa mwaka 1992 na umekuwa na miradi katika nchi 136 Duniani.

Post a Comment

0 Comments