WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amewaagiza Wakuu wote wa Mikoa wawahamasishe wananchi na wadau mbalimbali kutoa maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuisaidia timu ya kukusanya maoni kupata maoni yatakayoakisi mahitaji halisi ya nchi.
Pia amewaagiza Wakuu wote wa Mikoa washiriki kwenye mahojiano maalumu na kutoa maoni kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuhakikisha zoezi la uhamasishaji wananchi kushiriki kutoa maoni linafanyika kwenye kila halmashauri katika mikoa yao.
Ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Aprili 17, 2024) wakati akifungua semina ya Wakuu wa Mikoa kuhusu uelimishaji umma na uratibu wa zoezi la ukusanyaji maoni ya DIRA 2050 kwenye ukumbi wa Kambarage, HAZINA, jijini Dodoma.
Katika kuhakikisha kuwa zoezi la ukusanyaji maoni linafanikiwa, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar watoe ushirikiano wa kutosha kwa timu za wataalamu zitakazotembelea mikoa na wilaya kwa ajili ya ukusanyaji wa maoni kwa njia ya mahojiano na wananchi.
“Wakuu wote wa Mikoa zingatieni kuandaa vikao na watendaji katika ngazi zote za utawala na kuwapa elimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo pamoja na umuhimu wake,” amesema na kuongeza:
“Kwa kuwa mmepewa dhamana ya usimamizi wa zoezi hili katika mikoa yenu, nendeni mkawaelekeze na kuwasimamia Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, watendaji na viongozi wengine wa ngazi za kata/shehia, mitaa na vijiji pamoja na mabalozi na wajumbe wa nyumba kumi kumi, watoe ushirikiano kwa Mameneja Takwimu wa Mikoa na Makarani wa Dira 2050 katika ukusanyaji maoni ngazi ya kaya.”
Amesisitiza kuwa suala la kuhamasisha wananchi lipewe kipaumbele kinachostahili ili watambue umuhimu wa dira hii kwa ustawi na maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. “Vilevile, hakikisheni zoezi la ukusanyaji maoni linafanyika kwa amani na utulivu katika halmashauri zote zitakazofikiwa ndani ya mkoa.”
Amewataka wafanye ufuatiliaji wa zoezi hilo katika maeneo yao ya kiutawala na kutoa taarifa mara kwa mara sambamba na kuandaa ripoti za kila wiki ili iwe rahisi kufahamu mwenendo wa zoezi hilo.
Kuhusu ushiriki wa viongozi wa dini, Waziri Mkuu amewasihi wawahamasishe waumini wao kushiriki katika zoezi la kutoa maoni ya Dira mpya. “Mmekuwa wakati wote mkishirikiana na Serikali kutoa hamasa kuhusu masuala muhimu ya Kitaifa. Nitoe rai kwenu mshiriki kikamilifu katika utoaji maoni lakini pia kutoa hamasa kwa waumini wenu.”
Mapema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo alisema hadi sasa wananchi 623,614 tayari wametoa maoni kuhusu Dira ya Taifa kupitia kwenye mtandao (portal).
Amesema kuwa kati ya waliotoa maoni hayo, asilimia 70 ni wanaume huku idadi kubwa ya walijitokeza ikiwa ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15-35.
Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, alieleza hatua mbalimbali kuhusu mchakato wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, tangu ulipoanza 2021 hadi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipozindua mchakato wa ukusanyaji wa maoni Desemba 9, 2023 na hatua zilizofanyika hadi kufikia semina hiyo kwa Wakuu wa Mikoa.
0 Comments