About Me

header ads

KAMATI YA BUNGE YATAKA MIPANGO MATUMIZI YA ARDHI VIJIJINI KUSIMAMIWA

 

Na Munir Shemweta, RUANGWA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imeitaka mipango ya matumizi ya ardhi  inayotekelezwa katika vijiji mbalimbali nchini kusimamiwa ipasavgo na Kamati za Vijiji ili iweze kuleta tija katika vijiji husika.

Aidha, Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge imeipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kwa kazi nzuri inayoifanya kutekeleza miradi ya mipango ya matumizi ya ardhi kupitia Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi katika vijiji mbalimbali nchini.

Kwa mwaka 2023/2024 wizara ya ardhi kupitia Tume ya  Taifa ya Matumizi ya Ardhi na wadau wengine imewtekeleza miradi ya mipango ya matumizi ya ardhi katika  vijiji 333 kwa nchi nzima.

Mradi wa upangaji matumizi ya ardhi unatekelezwa na Wizara ya Ardhi kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ambayo imepewa jukumu kubwa kisheria la kuwezesha na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi mbalimbali nchini. Mipango hiyo huandaliwa katika ngazi ya Taifa, Kanda, Mikoa, wilaya na vijiji.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe, Timotheo Mzava akiwa katika ziara ya Kamati yake tarehe 13 Machi 2024 katika kijiji cha Namkatila halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi amesema, kupanga mipango ya Matumizi ya ardhi ni jambo moja na kuisimamia na kutekeleza ni jambo lingine.

Amebainisha kuwa, kazi ya kusimamia mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji siyo ya waziri, Tume na wala wakuu wa wilaya  na ndiyo maana zipo kamati za vijiji zilizotokana na wananchi wa vijiji husika.

"Niombe mipango ya matumizi ya ardhi  iliyotumia fedha za nchi na walipa kodi kuitengeneza ikasimamiwe na kuheshikiwa na wenzetu katika kamati wasaidie ili mipango hiyo  ikalete matokeo na matumda yaliyokusidiwa". Alisema Mhe, Mzava.

"Tukiwa na mipango tunajisifia tumeipanga halafu hatuifuati itakuwa ni kazi ya bure na huko vijjjini wenyevi na wenzake wakuendelea na ujanja ujanja wa kuuza maeneo bila kufuata mipango iliyopangwa hatuwezi kutoka na haiwezi kutusaidia" alisema Mhe, Mzava 

Awali Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amesema, utekelezaji wa miradi ya upangaji matumizi bora ya ardhi katika vijiji mbalimbali nchi ni juhudi za wizara yake kuona vijiji vyote vinakuwa katika mpangilio mzuri.

Amesema, kwa wilaya ya Ruangwa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi imeweza kutekeleza mradi katika vijiji 16 na kutaja baadhi ya vijiji hivyo kuwa ni Chikwale, Chihundu, Nambilanje, Mkaranga, Nanganga , chikoko na Likwachi.

Kwa mujibu wa Mhe, Pinda, Tume imewezesha uandaaji mipango kina wa maeneo ya makazi kwenye kijji cha Namkatila uliowezesha uandaaji wa hati za kimila 787 na upimaji mipaka ya vijiji 10 pamoja na upimaji mIpaka ya vijiji uliowezesha utatuzi wa migogoro ya mipaka ya muda mrefu hususan mgogoro wa moaka kati ya vijiji vya Nanjaru na Mnyangala vilivhopo katika manispaa ya Lindi.

Aidha, Mhe, Pinda ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi kwa utashi walionao na kueeleza kuwa, umetoa msukumo  wa kuongeza kasi ga uandaaji  mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji ambayo ni nyenzo muhimu katika utatuzi na udhibiti wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini inayoendelea kuwa kero kwa wananchi kwa muda mrefu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imefanya ziara ya  kukagua utekelezaji wa mradi wa kupanga matumizi ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Ruangwa . Aidha, Kamati pia ilikabidhi vyeti vya ardhi ya vijiji, ramani za mipaka iliyopimwa na kuhuishwa, mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji na Hati za Hatimiliki za kimila kwa wanaichi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii Mhe, Timotheo Mzava akizungumza katika mkutano na wananchi wa kijiji cha Namkatila katika hamashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 13 Machi 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akizungumza na wananchi wa kijiji cha Namkatila wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokwenda kukagua mradi wa upangaji mipango ya matumizi ya ardhi tarehe 13 Machi 2024.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemela akizungumza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokwenda kukagua mradi wa upangaji mipango ya matumizi ya ardhi katika kijiji cha Namkatila katika halmashauri ya Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 13 Machi 2024.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii Mhe, Timotheo Mzava akimkabidhi Daftari la Ardhi la Kijiji la Hati za Haki Milki za kijiji cha Namkatila katika hamashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge tarehe 13 Machi 2024.Mbunge wa Viti Maalum Asia Halamga akimkabidhi Hati Milki ya Kimila mmoja wa wananchi wa kijiji cha Namkatila katika halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 13 Machi 2024.Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akimkabidhi Hati Milki ya Kimila mmoja wa wananchi wa kijiji cha Namkatila katika halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 13 Machi 2024.Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemela akikabidhi Hati Milki ya Kimila kwa mmoja wa wananchi wa kijiji cha Namkatila wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii tarehe 13 Machi 2024.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Namkatila wakishuhudia ugawaji wa hati miliki za kimila wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii tarehe 13 Machi 2024 (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

 

Post a Comment

0 Comments