Na Munir Shemweta, CHALINZE
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imesema kuwa, haijaridhishwa na urejeshaji mikopo ya fedha za mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi (KKK) unaofanyika kwenye halmashauri mbalimbali nchini.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 18 Machi 2024 na Kamati hiyo wakati ilipotembelea na kukagua utekelezaji mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika eneo la Msolwa katika halmashauri ya wilaya ya Chalinze mkoa wa Pwani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe, Timotheo Mzava ameeleza kuwa, mbali na Kamati yake kuridhishwa na mradi wa KKK kwa ujumla lakini hawajaridhishwa na namna mikopo hiyo inavyorejeshwa na halmashauri.
Akitolea mfano wa Halmashauri ya Chalinze katika mkoa wa Pwani, Mhe, Mzava amesema pamoja na halmashauri hiyo kukopeshwa kiasi cha shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya mradi wa KKK lakini imeshindwa kurejesha fedha kwa wakati.
‘’Kama Kamati bado hatujaridhishwa kabisa namna ya kasi ya urejeshaji fedha hizi na wito na msisitizo wetu zifanyike kila aina ya jitihada kuhakikisha fedha zinarudi ili zikasaidie maeneo mengine yenye uhitaji ili dhamira ya Rais ya kutoa fedha hizo iweze kufikiwa’’ alisema Mzava
Kwa mujibu wa Mhe, Mzava, hadi Machi 2024 kwa ujumla wizara imepokea marejesho ya shilingi bilioni 22.7 kati ya shilingi bilioni 50 sawa na asilimia 45 kutoka kwenye halmashauri na taasisi mbalimbali zilizonufaika na mkopo huo.
Amesema, fedha zinazotolewea kama mkopo usio na riba kwa halmashauri zikirejeshwa zitasaidia kukopesha halmashauri nyingine na hivyo kuisaidia kutatua changamoto za sekta ya ardhi nchini na kuboresha katika maeneo mengine.
Hata hivyo, ametaka kufanyika jitihada mbalimbali ili kusaidia katika urejeshaji mikopo hiyo na kuweza kuzisaidia halmashauri nyingine ili ziweze kuondoa changamoto za sekta ya ardhi nchini.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amebainisha kuwa, mpaka sasa halmashaurii zilizorejesha kiasi chote cha fedha ya mkopo ni 12 huku zile zilizorejesha sehemu ya fedha zikiwa ni 43.
Mhe, Pinda amesema, Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) ni program ya miaka kumi inayotekelezwa na wizara yake kwa kushirikiana na halmashauri mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa, utekelezaji wa Programu hiyo ulianza mwaka 2018/2019 na unatarajiwa kukamilika 2028/2029. Lengo la Programu ya KKK ni Kupanga miji na kuhakikisha makazi holela yanaondolewa kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Programu hiyo inatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ambazo ni mamlaka za upangaji na sekta binafsi ambapo program hiyo inagharimiewa na serikali kupitia fedha za ndani za bajeti ya maendeleo.
Serikali ilitoa mtaji wa shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya utekelezaji wa program ya KKK kwa utaratibu wa kuzikopesha halmashauri na taasisi ambapo wizara kwa kushirikiana na wizara ya fedha na Ofisi ya Rais TAMISEMI ziliweka utaratibu kwa kuweka vigezo vya kutoa mkopo huo bila riba kwa ajili ya utekelezaji wa program.
0 Comments