Shirika la Posta Tanzania limekabidhi mifuko 300 ya Saruji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo Wilayani Tanganyika, Mkoa wa Katavi. Mifuko hiyo imekabidhiwa leo tarehe 8 Julai, 2023 na Mkurugenzi wa Huduma za Posta Ndugu Arubee Ngaruka kwa niaba ya Postamasta Mkuu.
Mifuko hiyo imepokelewa na Mkurugenzi ya wilaya ya Tanganyika Ndugu Shabani Juma ambaye amelishukuru Shirika la Posta kwa kuithamini Wilaya ya Tanganyika na kuwaletea mifuko ya Saruji kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
"Tulipeleka maombi Taasisi nyingi za kiserikali na binafsi kuomba tupatiwe vifaa mbalimbali vya ujenzi kwa ajili ya Shule, vituo vya afya, kituo cha polisi na miradi mingine mbalimbali ila tunalishikuru Shirika la Posta kwa kuwa wa kwanza kuitikia maombi yetu na kutupa msaada wa Saruji" alieleza Ndugu Shaban Juma.
Tukio hilo limefanyika huku likishuhudiwa na Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso ambaye ameeleza kufurahishwa kwake na namna Shirika hilo lilivyo karibu na jamii kupitia huduma zake, misaada yake kwa jamii huku akivitaka vijiji vilivyopokea saruji hiyo vikaitumie vizuri na kusiwepo na malalamiko yoyote ya upotevu wa Saruji hiyo.
Nae Mkurugenzi wa Shughuli za Posta, Ndugu Arubee Ngaruka, amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso kwa kuwa mstari wa mbele kulitangaza Shirika hasa kwenye mageuzi makubwa yaliyofanyika katika kipindi kifupi hivyo kuifanya Posta kusikika kwa wananchi.
Aidha Ndugu Arubee alitumia fursa hiyo kuwaeleza Wananchi wa Wilaya ya Tanganyika huduma zinazotolewa na Shirika hilo ikiwemo Usafirishaji wa haraka kupitia EMS, Usafirishaji wa kawaida wa Posta, Usafirishaji wa mizigo mikubwa kupitia "Post Cargo" na Duka mtandao la Shirika la Posta "Posta shop".
Shirika la Posta limekabidhi mifuko 300 ya saruji, ambapo mifuko 150 imepelekwa kwenye shule za vijiji vya Ngomalusambo, Majalila (Mpanda Ndogo) na Katobo(Silonge) kwa ajili ya ujenzi wa sakafu za madarasa, mifuko 100 imepelekwa katika vijiji vya Mgansa na Isubangala kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati, pamoja na mifuko 50 kwa ajili ya jengo la kituo cha Polisi la Mpanda Ndogo.
Shirika la Posta limekuwa mdau muhimu wa shughuli za jamii kupitia huduma zake za kila siku zinazogusa wananchi katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii, ambapo kupitia wapitia wadau na wateja wake, Shirika limeweza kukua kimapato na kiuchumi siku hadi siku hivyo utoaji wa mifuko hiyo ya saruji ni sehemu ya Shirika kurudisha fadhila kwa jamii inayolizunguka na kulitumia Shirika hilo.
Mkurugenzi wa Huduma za Posta, Ndugu Arubee Ngaruka (wa pili kushoto) akikabidi mifuko 300 ya saruji iliyotolewa na Shirika la Posta kwa ajili kujenga Shule, Zahanati na Kituo cha Polisi Wilayani Tanganyika, Mkoa wa Katavi.
Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso akizungumza wakati wa akipokea mifuko 300 ya saruji iliyotolewa na Shirika la Posta Tanzania kwa vijiji vilivyopo Wilaya yaTanganyika, Mkoa wa Katavi.
Mkurugenzi ya Wilaya ya Tanganyika Ndugu Shabani Juma akizungumza wakati wa kupokea mifuko 300 ya saruji iliyotolewa na Shirika la Posta Tanzania kwa vijiji vilivyopo Wilaya yaTanganyika, Mkoa wa Katavi.
Mkurugenzi wa Huduma za Posta Ndugu Arubee Ngaruka kwa niaba ya Postamasta Mkuu akizungumza wakati wa kukabidhi mifuko 300 ya Saruji katika Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi.
0 Comments