NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF)
umewatahadharisha Wanachama wake hususan Wastaafu kuwa makini kufuatia aina
mpya ya utapeli ambapo wahalifu wa kimtandao wamekuwa wakiwalaghai Wastaafu
wanaopokea Pensheni ya kila mwezi.
Tahadhari hiyo imetolewa leo Julai 2, 2023 na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe ikiwa ni sehemu ya Elimu kwa Wanachama inayotolewa kwenye banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Wahalifu
wa kimtandao wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za kihalifu na sasa wamebuni
ujumbe mfupi wa simu (sms) na kumtumia Mstaafu wakimueleza kuwa akaunti yako
imefungwa na hivyo kumuelekeza atume taarifa za akaunti yake kwenye namba
ambayo usipoiangalia kwa umakimni utaamini kuwa ni namba maalum na siyo ya simu
ingawa kimsingi ni namba ya simu, na mstaafu anapotekeleza maelekezo hayo
wahalifu wanaingia kwenye akaunti na kuchukua fedha zilizopo.” Alifafanua Bw.
Mlowe.
Alisema awali wahalifu hao wa
kimtandao walikuwa wanawatapeli wastaafu wakishalipwa kiinua mgongo (Lumpsum
Payment) ambapo waliwalaghai kwa kuwaeleza kuwa malipo yao waliyopokea
ni pungufu kwa hivyo wao wana uwezo wa kufanya marekebisho ili wapate malipo
zaidi wanayostahili.
“Hata hivyo utapeli huu umegonga
mwamba baada ya kuwapa elimu ya kutosha wastaafu wetu na ndio maana wamebuni
mbinu hii mpya.” Alisema.
Bw. Mlowe amewatahadharisha
Wanachama na Wastaafu kutopokea maelekezo yoyote kutoka kwa watu wasiowafahamu
wanaotaka kujua kuhusu malipo yanayofanywa na PSSSF.
“Tuna ofisi kila mahali Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, kwa hivyo Mwanachama kama una jambo lolote
usilolifahamu kuhusiana na malipo yako wasiliana na ofisi zetu moja kwa moja
bila ya kupitia kwa mtu yeyote usiyemfahamu.” Alisisitiza Meneja Huyo wa Uhusiano
na Elimu kwa Wananchama.
Aidha mmoja wa wanachama wa PSSSF
ambaye anakaribia kustaafu, Mwalimu wa Shule ya Msingi Msasani jijini Dar es
Salaam, Bw. Osmund Xavery Hyera, alisema visa vya utapeli kwa wastaafu hata
yeye amevisikia na kutoa ushuhuda kuwa mwalimu mwenzake (hakumtaja jina),
aliwahi kupigiwa simu wakati akikaribia kupokea mafao ya mkupuo.
“Walimueleza kuwa wao wanauwezo wa
kuharakisha Mchakato wa malipo yake kwahiyo wakamtaka atoe taarifa
zitakazowezesha zoezi hilo kufanyika." Alisema Mwalimu Hyera
Alisema " Hao matapeli walijitambulisha wako TAMISEMI Dodoma, bahati nzuri mtoto wa yule mstaafu akamwambia baba yake asifanye mawasiliano yoyote na kumuachia jukumu hilo alifanye yeye kuwasiliana na watu hao, alipowataarifu kuwa kuwa amefika TAMISEMI ili kupata ufafanuzi walikata simu.” Alifafanua.
Aidha kuhusu ushiriki wa Mfuko kwenye Maonesho hayo yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Tanzania Mahali Salama kwa Biashara na Uwekezaji.” Bw. Mlowe alisema, Wanachama, Wastaafu na Wananchi kwa ujumla wanahimizwa kutembeela banda la PSSSF ili kupata elimu ya hifadhi ya jamii kama vile Taarifa za Michango ya Wanachama, Taarifa kuhusu Mafao mbalimbali yatolewayo na Mfuko, Taarifa za Uwekezaji na fursa mbalimbali zinazopatikana PSSSF na kwa Wastaafu wataweza kujihakiki.
“Sheria inataka Mstaafu kujihakiki mara moja Kila Mwaka, safari hii tuna utaratibu mpya na wakisasa unaomuwezesha Mstaafu kujihakiki." Alisema
Zamani Mstaafu alilazimika ku Eva nyaraka wakati anakuja Ofisi za PSSSF kujihakiki, tumeachana na mfumo huo hivi sasa Mstaafu atalazimika kuja na kitambulisho chake cha NIDA au namba ya NIDA na atachukuliwa alama zake za vidole (biometric) na tayari atakuwa amejihakiki na ni mara moja tu kwa Mwaka, Alifafanua Bw. Mlowe.
Sambamba na kuwahudumia wanachama na
wastaafu kwenye banda la Mfuko, PSSSF pia imekuja na staili mpya ya kuwatembelea wanachama wake ambao ni watumishi wa Umma wanaoshiriki kwenye
maonesho hayo huko huko waliko kwenye mabanda yao kampeni inayokwenda kwa jina
la “Banda kwa Banda”.
“Tumeona ni njia nzuri ya
kuwahudumia wanachama wetu waliopo hapa Sabasaba, kwa kuwa na wao wanatoa
huduma kwa wananchi, sisi tunawafuata huko huko waliko na kuwaelimisha kuhusu
matumzi ya huduma za PSSSF Kiganjani na PSSSF ulipo Mtandao.” Alisema Bw. Abdul
Njaidi, Afisa Uhusiano Mkuu PSSSF.
Alisema huduma hiyo humfanya mtu
anayekabiliwa na majukumu mengi kupata huduma za PSSSF kupitia simu yake ya
kiganjani kwa kupakua APP ya PSSSF kwenye simu yake.
“Lakini kampeni hii ya Banda kwa Banda imetuwezesha kugundua kuwa baadhi ya wanachama wetu wanahitaji ufafanuzi tu ili kutatua changamoto ndogo ndogo zinazowakabili kuhusiana na huduma zetu.” alibainisha Bw. Njaidi.
0 Comments