Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO)limesema linatambua nafasi ya wanawake na akina mama katika: uhifadhi wa mimea dawa,malezi ya maadili ya jamii,* Matumizi sahihi ya tiba asili na ulinzi wa mazingira.
TRAMEPRO imeyasema hayo kupitia Katibu Mkuu wake Boniventura Mwalongo wakati wakitoa salamu katika Maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani.
Mwalongo amesema Shirika hilo linatoa salamu za heshima, upendo na pongezi kwa akina mama wote duniani katika maadhimisho hayo ambayo huadhimishwa duniani kote kila Jumapili ya pili ya mwezi Mei.
Ameongeza lengo ni kuthamini mchango mkubwa wa mama katika malezi, ustawi wa familia, maadili ya jamii na maendeleo ya Taifa. Historia inaonyesha kuwa maadhimisho haya yalianzishwa kupitia juhudi za Anna Jarvis nchini Marekani mwanzoni mwa karne ya 20, kama njia ya kutambua upendo, kujitoa na nafasi ya mama katika maisha ya mwanadamu.
"Katika maadhimisho haya ya mwaka 2026, tunawakumbusha wananchi kuendelea kuwaheshimu, kuwathamini na kuwaenzi akina mama kwa mchango wao mkubwa katika jamii, afya, malezi, elimu, kilimo, mazingira na maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho."
Pia amesema TRAMEPRO inaamini kuwa jamii yenye kuwathamini wanawake na akina mama ndiyo msingi wa Taifa lenye maadili, afya njema na maendeleo endelevu.
Kauli ya kutafakari mwaka 2026: “Upendo wa Mama ni msingi wa familia imara na jamii yenye utu.”
" Mungu awabariki akina mama wote duniani.
Mungu ailaze roho ya marehemu mama yangu mzazi Ostela Sanga mahali pema peponi. Amina."


0 Comments