NAIBU WAZIRI wa afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kusimamia huduma za afya ya mama na mtoto na kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kuanzia zahanati mpaka hospitali ya Rufaa ya taifa kuwa na dirisha maalumu kwaajili ya kuwahudumia wazee ili kuepusha usumbufu unaowakumba.
Ametoa wito huo leo Juni 1, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Mhe. Bupe Nelson Mwakang'ata katika Bunge la kumi na mbili Mkutano wa kumi na moja kikao cha 38, Jijini Dodoma.
"Kwenye swala la wazee tumeagiza kila kitu cha afya, kila zahanati na kila hospitali kuwepo na dirisha kwaajili ya kuwahudumia wazee, na tunaomba wenzetu Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wasimamie ili eneo ili kuhakikisha takwa la kisera linatekelezwa ipasavyo." Amesema Dkt. Mollel.
Ameendelea kusema, katika kuhakikisha Sera ya afya inatekelezwa vizuri Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga zaidi ya Bilioni 167 ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu ikiwemo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba utaoenda kutatua changamoto ya huduma kwa wazee na mama na mtoto nchini.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel ametoa wito kwa watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya kutowatoza gharama za uzazi wanawake wote wanaofika vituoni kupata huduma ya afya ya uzazi kwani Sera ya Afya ya mwaka 2007 kifungu Na. 5.3.4C (i) kinaelekeza kuwa huduma za afya ya uzazi kuanzia kipindi cha kliniki mpaka baada ya kujifungua hutolewa bila malipo.
0 Comments