About Me

header ads

CDC kupitia THPS wameimarisha utoaji wa huduma ya Kuzuia saratani ya mlango za kizazi

 


Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi Maria Mpongwe akizungumza na waandishi habari kuhusiana ufadhili wa CDC kupitia THPS walivyoweza kuimarisha utoaji wa huduma ya Saratani ya Mlango wa Kizazi. 
Afisa mradi wa Afya ya Uzazi ya Mama Mtoto wa THPS Mkoa wa Pwani Dkt. Asnath Nnko akizungumza na waandishi habari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi kuhusiana na uimarishaji wa huduma ya kuzuia saratani ya Saratani ya Mlango wa Kizazi.
Mtaalam wa Maabara Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Innocent Kweka akizungumza namna CDC kupitia THPS walivyorahisisha kuhusiana na upimaji na uchukuaji wa majibu ya kimaabara kwenye utoaji wa huduma ya Saratani ya Mlango wa Kizazi.

*Ni akina mama wenye dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi.

Na Chalila Kibuda, Michuzi TV Pwani
TANZANIA Health Promotion Support (THPS) kwa ufadhili wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa UKIMWI (PEPFAR) kupitia Shirika la CDC wameimarisha utoaji wa huduma ya Kuzuia saratani ya mlango za kizazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kwa kutibu wanawake walio na dalili za awali za saratani hiyo

Akizungumza katika ziara ya waandishi waliotembelea hospitali hiyo Afisa mradi wa Afya ya Uzazi ya Mama Mtoto wa THPS Mkoa wa Pwani Dkt. Asnath Nnko amesema kuwa THPS kupitia mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua imeweza kuimarisha utoaji wa huduma hizo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani- Tumbi kwa kutoa vifaa vya kisasa vya kuchunguza saratani ya mlango wa kizazi na kutoa tiba mgando kwa wamama wenye dalili za awali na wengine wenye kuhisiwa kuwa na saratani ya mlango wa kizazi hupewa rufaa kwenda katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Dkt.Asnath amesema kuwa dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi ni pamoja na mwanamke kutokwa na baka katika shingo ya kizazi ila anapobainka mapema na kutibiwa hupona kabisa.

Amesema kuwa awali Mradi wa Afya Hatua ulilenga kutoa huduma hizo kwa wanawake wenye virusi vya UKIMWI lengo likiwa ni kuimarisha ufubavu wa VVU lakini kutokana na umuhimu wa huduma hizi kwa sasa wanawake wote wanaofika Tumbi hospitali kutaka huduma hizi hufanyiwa uchunguzi pia.

Aidha amesema kuwa kabla ya THPS kupitia ufadhili wa CDC kuanza kutoa huduma hizi wanawake wengi walishindwa kumudu gharama za vipimo vya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi lakini sasa huduma hiyo hutolewa bila malipo kwa wanawake wote katika hospitali hiyo.

Aidha Dkt. Asnath ameongeza kuwa kwa wanawake wanaohisiwa kuwa na saratani hiyo hutolewa vinyama ambavyo hupelekwa katika Hospitali ya Mloganzila kwa uchunguzi na THPS kupitia ufadhili wa PEPFAR/CDC hulipia gharama zote za kipimo cha “biopsy”

Amesema kufikia mwezi Machi, 2023 jumla ya wanawake 58 waliokuwa na baka kwenye mlango wa uzazi walipimwa na kupatiwa tiba mgandisho. Kadhalika wahisiwa wa saratani 27 walifanyiwa kipimo cha biopsy na walipewa rufaa kwenda Ocean Road kwa matibabu zaidi

Post a Comment

0 Comments