CHAMA cha Hisabati Tanzania (MAT/CHAHITA ) kimetoa taarifa ya mtihani ya mashindano ya hisabati ya Afrika Mashariki kwa ushiriki wa Tanzania huku kikileza lengo kuu la mashindano hayo ni kuongeza uelewa, utayari na ufaulu wa hisabati.
Malengo mengine ni kuongeza motisha kwa wanafunzi kupenda hisabati (Matokeo na zawadi) na kuleta ushindani katika mbinu za kufanya maswali ya hisabati.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mkuu wa Idara ya Hisabati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mlezi wa chama cha Hisabati Dkt.Sylyvester Rugeihyamu
amefafanua kuwa Chama hicho kilianzishwa mwaka 1966 katika Idara ya Hisabati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na lengo kuu ni kuendeleza kwa ufanisi somo la Hisabati hapa Tanzania kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau.
Amesema pamoja na shughuli zingine, chama pia kinaratibu mashindano ya Hisabati kwa ngazi za kitaifa na kimataifa ikiwa ni sehemu ya kutimiza malengo yake. Kila mwaka chama huandaa mitihani ya mashindano ya kitaifa kwa makundi ya sekondari (O-level na A-level) yajulikanayo kwa jina la Junior and Senior Contests.
“Mitihani hii ya mashindano hufanyika kila Oktoba ya kila mwaka na matokeo yake hutangazwa na washindi hupewa zawadi katika Siku ya Hisabati Duniani (IDM) kwa mwaka unaofuata Machi 14. Hata hivyo mbali na mashindano ya Kitaifa, washiriki na hasa waliofaulu vizuri huweza kushiriki mitihani ya mashindano ya Kimataifa. Mitihani ya kimataifa iko aina tatu ambayo ni; Afrika Mashariki (EAMO), Afrika (PAMO) na ya Dunia (IMO)",amesema Dkt Rugeihyamy.
Akieleza zaidi amesema malengo mengine ya mashindano kuweza kutambua vipaji mapema kwa wanafunzi na kuendelezwa,kutathmini uwezo wa wanafunzi katika mbinu za kupata majibu ya maswaliili waweze kusaidiwa zaidi na walimu wao,kuchochea na kutambua ubunifu na uvumbuzi kwa wanafunzi kupitia mitihani.
Pia kujenga ushirikiano wa kitaaluma na mataifa mbalimbali duniani kwa wanafunzi na Walimu .Kuhusu Mitihani ya Mashindano ya Afrika Mashariki (EAMO) amesema Aprili 20 mwaka huu kulifanyika mitihani ya Mashindano ya Afrika Mashariki ambapo nchi saba zilishiriki ikiwemo Tanzania.
Kwa upande wake Katibu Taifa wa MAT/CHATITA Dkt. Said Sima amesema Mitihani hiyo iliratibiwa Rwanda kwa kila nchi kufanya mitihani kwa muda moja katika nchi husika ikiwa na uangalizi wa picha kupitia teknolojia ya mikutano ya zoom. Nchi zilizoshiriki ni Tanzania, Rwanda, Kenya, Uganda, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini na kwamba kila nchi ilitoa washiriki saba naTanzania walikuwa na washiriki sita
“Washiriki wa Tanzania ambao ni wale ambao walikuwa washindi Wamitihani ya MAT/CHAHITA (Junior Contest 2022)na washindi wawili kwa upande wawasicha.Washiriki hao ni Hamza Mwangadu Mwamotto (Feza Boys), Derick Evarist Kasumbai (Feza Boys),.Haris Israel Phares(Feza Boys), Mwanamis Mashauri Halidi( Inspire sec), Blessing Edward Masanga(Mbeya Sec) na El-Gibbor Evance Tweve( Mbeya Sec).
“Matokeo ya Mitihani hii yalitangazwa Aprili 22 mwaka huu ambako kulikuwa na washindi 4 wa medali ya Dhahabu (Nafasi ya kwanza),washind iwa medali ya Fedha(Nafasi yaPili) na 9 washindiwa medali ya Chuma(Bronze) (nafsi ya Tatu) 12. Tanzania tumepata mshindi wa tatu ambaye ni Haris Israel Phares aliyekuwa mwanafunzi wa Feza Boys aliyemaliza kidato cha nne,2022.Mashindano haya yameanzishwa mwaka jana na sisi tumeshiriki kwa mara ya kwanza,2023.”
Aidha amesema kutakuwa na mitihani ya PAMO 2023 itakayofanyika Kigali–Rwanda Mei 15 hadi Mei 22, 2023 na watakuwa na washiriki sita 6 ambapo watatu ni Wavulana na watatu wasichana) wakati mitihani ya Mashindano ya Kitaifa 2023(O-level na A-level) itafanyika kwa vituo maalum katika maeneo ya Bagamoyo,Morogoro,Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.
Wakati huo huo Mzazi wa Haris, ambaye amefanya vizuri kwenye mashindano hayo, Bw.Phares Magesa amekipongeza chama cha Hisabati Tanzania (MAT/ CHAHITA) kwa kuandaa mashindano hayo ambayo yanaweza kuonesha kwamba Tanzania pia kuna vipaji ambavyo vinaweza vikashindana na kwenda kimataifa.
Magesa amewahakikishia wadau mbalimbali kwamba mtoto wake ambaye ni mshindi anaweza kufika mbali kimataifa kwani uwezo huo anao na anaamini atafanikiwa.
Pamoja na hayo Magesa ametoa wito kwa wazazi na walezi kwamba waendelee kujitahidi kutoa ushirikiano kwa watoto wao pale inapohitajika kuwasaidia ili waweze kufikia malengo yao katika maisha.
Mkuu wa Idara ya Hisabati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mlezi wa chama cha Hisabati Dkt.Sylyvester Rugeihyamu alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam wakati akiwatangaza wanafunzi washindi wa Shindano la Hisabati kwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Kusini.,Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama cha Hisabati Tanzania Dkt.Said Sima
Katibu Taifa wa MAT/CHATITA Dkt. Said Sima akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam wakati wa kuwatangaza wanafunzi washindi wa Shindano la Hisabati kwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Kusini,kulia ni Mkuu wa Idara ya Hisabati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mlezi wa chama cha Hisabati Dkt.Sylyvester Rugeihyamu
0 Comments