Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameziagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuhakikisha wanakaa pamoja ili kutatua masuala mbalimbali ikiwemo changamoto ya kusomana kwa mifumo hususani katika eneo la Bandari.
Dkt. Samia ametoa agizo hilo wakati akipokea Ripoti ya mwaka 2021-2022 ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zoezi lililofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
“TPA na TRA kaeni kitako na hakikisheni mifumo inasomana, Bandarini kuna tatizo la siku nyingi la mifumo kushindwa kusomana, Bandari ni lango kuu ambalo linaweza kuchangia nusu ya pato la taifa letu,” amesema Dkt. Samia
“Karibisheni Sekta Binafsi ili wasaidie kuimarisha mifumo ili mifumo hiyo isomane vizuri, nimeongea siku nyingi sana kama mifumo isiposomana maana yake mnafanya makusudi. Nasikia kuna Wataalamu wa mifumo, raia wa Korea, Waziri wa Fedha hakikisheni Wataalamu hao hawaondoki ili wasaidie mifumo hiyo kusomana,” ameeleza Dkt. Samia
Awali, akiwasilisha Ripoti hiyo ya TAKUKRU mbele ya Rais Samia, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP. Salum Hamduni amesema Taasisi hiyo imefanya uchambuzi wa vihatarishi vya rushwa katika eneo hilo la Bandari na matokeo yamebaini yenye vihatarishi vya rushwa kuwan ni eneo la Forodha, eneo la ubebaji mizigo, mapato katika Bandari, na ukaguzi unafanywa na Taasisi za Shirika la Viwango nchini (TBS), Kilimo, Misitu na Mawasiliano na TANROADS.
Aidha, CP. Hamduni amesema katika uchambuzi huo umebaini kuwa vihatarishi hivyo vya rushwa vinasababishwa na masuala ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Wateja kutojua taratibu za kufuata ili kupata huduma, uwajibikaji hafifu wa baadhi ya Watendaji wa Mamlaka na fikra potofu za baadhi ya watumishi wa Mamlaka kwamba eneo hilo ni sehemu ya kuchuma fedha.
0 Comments