About Me

header ads

SERIKALI KUANZISHA MAMLAKA YA MILKI TANZANIA

Na Munir Shemweta


Serikali iko mbioni kuanzisha Mamlaka ya Milki Tanzania kwa lengo la kuimarisha usimamizi, udhibiti na uendelezaji wa sekta ya milki nchini.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, amebainisha hayo leo Novemba 23, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao kazi cha Wizara ya Ardhi na kampuni zinazojihusisha na mipangomiji, upimaji ardhi na uendelezaji wa milki nchini.

Amesema, Serikali inahitaji kuwa na chombo chenye mamlaka kamili ya kisheria kitakachoweza kusimamia na kuendeleza sekta ya milki ili kuhakikisha inakuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kwa sasa Serikali hainufaiki kikamilifu na sekta ya milki kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo baadhi ya shughuli kufanyika kwa kificho na kukosekana kwa mfumo madhubuti wa usimamizi.

Ameeleza kuwa, takwimu zinaonesha sekta ya milki inachangia asilimia 4.4 pekee katika uchumi wa taifa, kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na baadhi ya nchi nyingine ambako sekta hiyo inachangia zaidi ya asilimia saba.

“Hapa tunakosa pesa nyingi kutokana na kukosekana kwa mamlaka kamili ya kuisimamia sekta hii ya milki,” amesema Dkt. Akwilapo.

Akizungumzia zoezi la urasimishaji wa makazi holela nchini, Waziri Dkt. Akwilapo amesema programu hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuzuia na kudhibiti ongezeko la makazi yasiyopangwa aliyoyaeleza kuwa hayatoi taswira nzuri ya miji sambamba na kuathiri maendeleo ya miji hiyo.

Amesema, Serikali itaendelea kusimamia urasimishaji wa makazi holela ili kuwezesha nchi kuwa na makazi bora, salama na endelevu, huku akizitaka kampuni na wadau wa kutumia fursa zilizopo kuboresha makazi bila kuathiri maisha ya wananchi.

“Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi kwa kuwa sekta hiyo imekuwa ikishiriki kwa kiasi kikubwa katika miradi mingi kama vile uwekezaji, nyumba na biashara,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Lucy Kabyemera, amesema kikao kazi hicho kinalenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Urasimishaji, Sekta ya Milki, Upangaji na Upimaji wa Ardhi.

Amesema, majadiliano hayo yanatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha maendeleo ya makazi, ujenzi wa nyumba bora na kuwezesha nchi kuwa na mipango mizuri ya matumizi ya ardhi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

“Hiki kikao kazi kitakuja na mapendekezo ya kuboresha maendeleo ya makazi, ujenzi wa nyumba bora na kuwa na nchi iliyopangwa vizuri kuelekea Dira ya 2050,” amesema.

Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Wataalamu wa Mipangomiji TP Averist Mfinanga, amesema kampuni za mipangomiji zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Hata hivyo, amesema kampuni hizo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazofanya baadhi yake kushindwa kujiendesha kwa ufanisi.

Ametaja changamoto mojawapo kuwa ni kutolipwa kwa wakati au kutolipwa kabisa kwa huduma za urasimishaji wa makazi zinazotolewa kwa wananchi.

Naye Makamu wa Rais wa Chama cha Wapima Tanzania Bw. Simon Chuwa, amesema mabadiliko ya gharama za urasimishaji mara kwa mara bila kufanyika kwa utafiti wa kina yamesababisha baadhi ya kampuni kupata hasara kubwa.

Ameshauri Serikali na wadau kufanya utafiti wa kina ili kubaini gharama halisi za urasimishaji zitakazowezesha kampuni kutoa huduma kwa ufanisi na kuendelea kujiendesha kibiashara.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kinawakutanisha wataalamu kutoka kampuni za mipangomiji, upimaji wa ardhi na uendelezaji wa milki, na kinatarajiwa kuhitimishwa Novemba 24, 2026.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, akizungumza wakati wa kikao kazi cha Wizara ya Ardhi na kampuni zinazojihusisha na mipangomiji, upimaji ardhi na uendelezaji wa milki nchini kilichofanyika tarehe 23 Novemba 2026 jijini Dar es Salaam.






Sehemu ya washiriki wa kikao kazi kati ya Wizara ya Ardhi na kampuni zinazojihusisha na mipangomiji, upimaji ardhi na uendelezaji wa milki nchini kilichofanyika tarehe 23 Novemba 2026 jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Nyumba na Viwanja Bw. Kassim Ng’ombe wakati wa kikao kazi cha Wizara ya Ardhi na kampuni zinazojihusisha na mipangomiji, upimaji ardhi na uendelezaji wa milki nchini kilichofanyika tarehe 23 Novemba 2026 jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu Bi. Lucy Kabyemera.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, akiwa katika picha ya Pamoja na washirikia wa kikao kazi cha Wizara ya Ardhi na kampuni zinazojihusisha na mipangomiji, upimaji ardhi na uendelezaji wa milki nchini kilichofanyika tarehe 23 Novemba 2026 jijini Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Bi. Lucy Kabyemera (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)



Post a Comment

0 Comments