Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limetoa wito wa hatua za haraka za kuzima moto mkubwa unaoendelea kuteketeza mashamba katika Wilaya ya Makete, Mkoa wa Njombe, huku maisha ya wananchi, makazi, vyanzo vya maji na mazingira yakiwa hatarini.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 24, 2026, moto huo ulianza Oktoba 22, 2026, majira ya saa 2:30 usiku, katika eneo la Shule ya Sekondari Lupaseko, na kuathiri maeneo ya Kijiji cha Ikonda na Kijiji cha Ihera, Kitongoji cha Tagara.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa juhudi za kuuzima moto zinaendelea kwa kutumia njia za kienyeji, huku kukiwa na hofu ya madhara zaidi kwa wananchi, mali zao na viumbe hai.
Kutokana na hali hiyo, TRAMEPRO imeziomba Serikali ya Mkoa wa Njombe, uongozi wa Wilaya ya Makete, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na mamlaka nyingine zinazohusika kufika eneo la tukio haraka ili kuratibu operesheni ya kuzima moto na kuzuia uharibifu zaidi.
Aidha, shirika hilo limewataka wananchi kuchukua tahadhari na kuepuka kujiweka katika hatari wanaposhiriki katika juhudi za kuuzima moto huo.
TRAMEPRO imesisitiza umuhimu wa hatua za dharura ili kulinda maisha ya wananchi, mali zao na mazingira.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura Mwalongo.

0 Comments