About Me

header ads

TPSF YATAKIWA KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI KWA TIBA ASILIA

Dar es Salaam, Tanzania

Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limetoa pongezi kwa viongozi wapya wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), huku likitoa wito wa sekta ya tiba asilia kupewa nafasi katika mifumo ya uwakilishi, majadiliano ya sera na fursa za uwekezaji nchini.

Katika taarifa yake, TRAMEPRO limempongeza Bi. Angelina Ngalula kwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa TPSF, pamoja na Bw. Jitu Soni, Makamu wa Rais anayewakilisha Tanzania Bara, na Bw. Ali Amour, Makamu wa Rais anayewakilisha Zanzibar.

Uchaguzi huo umefanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 24 wa Mwaka wa TPSF uliofanyika Oktoba 16, 2026.

TRAMEPRO imewatakia viongozi hao mafanikio katika kutekeleza majukumu yao, ikieleza kuwa inatarajia uongozi huo kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali, pamoja na kukuza uwekezaji, ubunifu na fursa za kiuchumi kwa Watanzania.

Akizungumzia umuhimu wa sekta ya tiba asilia, Katibu Mkuu wa TRAMEPRO na Mtaalamu wa Tiba Asilia, Boniventura F. Mwalongo, amesema sekta hiyo ina mchango muhimu katika afya ya jamii, uhifadhi wa mazingira na mimea ya dawa, utafiti wa maarifa ya jadi, uzalishaji wa bidhaa na utalii wa tiba.

Amesema sekta hiyo pia inaweza kuwa chanzo cha ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi iwapo itawezeshwa kupitia sera rafiki, utafiti wa kisayansi, viwango vya ubora na mifumo madhubuti ya usimamizi.

TRAMEPRO imeeleza kuwa ushirikiano kati ya TPSF, Serikali, taasisi za utafiti, wataalamu wa tiba asilia na wadau wa mazingira unaweza kufungua fursa mpya za uwekezaji na biashara, huku ukilinda maarifa ya jadi na haki za wamiliki wake.

Shirika hilo limeitaka TPSF kuipa sekta ya tiba asilia nafasi katika majukwaa ya majadiliano ya sekta binafsi, programu za kuwawezesha wajasiriamali, upatikanaji wa mitaji na mafunzo ya biashara, pamoja na ujenzi wa viwanda vya bidhaa za tiba asilia vinavyokidhi viwango vya usalama na ubora.

“Sekta ya tiba asilia isiwe pembezoni mwa uchumi wa taifa, bali iwe sehemu ya majadiliano na fursa za maendeleo ya sekta binafsi Tanzania,” imeeleza TRAMEPRO katika taarifa hiyo.

Shirika hilo limethibitisha utayari wake wa kushirikiana na uongozi mpya wa TPSF katika kujenga uchumi jumuishi, kuendeleza ubunifu wa Kitanzania na kulinda afya ya watu na mazingira.

Kaulimbiu ya TRAMEPRO: Umoja wetu ndiyo nguvu yetu.

Imetolewa na:

Boniventura F. Mwalongo
Katibu Mkuu na Mtaalamu wa Tiba Asilia

Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) 

Post a Comment

0 Comments