About Me

header ads

WAZIRI AKWILAPO AZINDUA KLINIKI YA ARDHI YA KIDIJITI MTWARA

Na Munir Shemweta, WANMM MTWARA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amezindua rasmi Kliniki ya Ardhi kidijiti mkoani Mtwara huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata elimu na huduma mbalimbali za ardhi, ikiwamo upimaji, upangaji na umilikishaji.

Uzinduzi huo umefanyika Septemba 25, 2026 katika Uwanja wa Mashujaa Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo Dkt. Akwilapo alikabidhi Hatimilki 10 kwa wananchi na hati 75 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.

Amesema, Kliniki ya Ardhi ya kidijiti inatoa huduma za ardhi kwa njia ya kidijiti sambamba na kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi.

Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo, huduma hizo za kidijiti kwa sasa zinapatikana mikoa 17 ya Tanzania Bara na kuitaja kuwa ni Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Kagera, Arusha, Tanga na Kilimanjaro.

"Wizara inaendelea na maandalizi ya kuingiza mikoa 9 iliyosalia kwenye mfumo huo na baada ya mikoa hiyo kuingizwa, huduma za mfumo wa e-Ardhi zitakuwa zimeenea nchini kote" amesema.

Aidha, amewakumbusha wamiliki wa ardhi kutimiza wajibu wao wa kulipa Kodi ya Pango la Ardhi kwa wakati, akisema maendeleo hayawezi kutenganishwa na wajibu huo wa kulipa kodi.

“Tunapoongelea maendeleo lazima tujue jukumu la msingi kulipa kodi ya pango la ardhi,” amesema.

Ameongeza kuwa, ulipaji wa kodi kwa wakati utasaidia wananchi kuepuka usumbufu unaoweza kusababishwa na riba au hatua za kufutiwa umiliki.

Waziri huyo wa Ardhi amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini wanaotoa huduma katika Kliniki za Ardhi zinazoendelea kuzingatia utu, weledi na kutoa huduma kwa wakati.

Ameonya kuwa Wizara yake haitasita kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi watakaokwenda kinyume na misingi ya utoaji huduma bora.

"Wizara ya Ardhi itaendelea kuboresha utoaji huduma za ardhi huku akibainisha kuwa changamoto ambazo hazitaweza kutatuliwa wakati wa kliniki zitawekewa utaratibu maalumu wa kuzifanyia kazi" ameeleza.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amesema matumizi ya mfumo wa e-Ardhi yatarahisisha upatikanaji wa hatimiliki za ardhi kwa wananchi.

Amesema awali wananchi walikabiliwa na mlolongo mrefu katika kupata hati za ardhi katika mfumo wa makaratasi, lakini mfumo wa kidijiti umeleta mabadiliko kwa kurahisisha na kuharakisha huduma.

“Awali mlolongo ulikuwa mrefu wakati wa hati za makaratasi, lakini sasa mambo yako mkononi, mambo yanaenda kwa haraka,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Fraterny Hassan, amesema lengo la mfumo wa e-Ardhi ni kupunguza gharama na muda wanaotumia wananchi kufuatilia huduma za ardhi.

"Mfumo huu unaongeza uwazi kwa kuwa mwananchi anaweza kufuatilia maombi yake hatua kwa hatua bila kulazimika kufika ofisini" amesema.

Kwa mujibu wa Hassan, mfumo pia unafupisha muda wa utoaji huduma kwa kuwa maombi yanawafikia maafisa husika na mfumo unaelekeza hatua inayopaswa kufanyika.

Kliniki ya Ardhi Kidijiti inaendelea kutolewa katika mikoa mbalimbali nchini, ambapo baada ya uzinduzi wa kitaifa, mikoa yote itaendelea kutoa huduma za Ardhi Kliniki hadi tarehe 3 Oktoba 2026, kwa lengo la kuwafikia wananchi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi ya Kidigiti katika uwanja wa Mashujaa Manispaa ya Mtwara Mikindani Sept 25, 2026.


Sehemu ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi ya Kidigiti iliyozinduliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo katika uwanja wa Mashujaa Mtwara Sept 25, 2026
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Fraterny Hassan akielezea matumizi ya Mfumo wa Kidigiti wa e- Ardhi wakati wa Uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi ya Kidigiti katika uwanja wa Mashujaa Manispaa ya Mtwara Mikindani Sept 25, 2026.


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akikabidhi Hati Milki za Ardhi kwa wananchi wa Mtwara mara baada ya kuzindua rasmi Kliniki ya Ardhi ya Kidigiti kwa wananchi wa Mtwara katika uwanja wa Mashujaa Sept 25, 2026.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Newala Bw. Duncan Thebas mara baada ya kumkabidhi Hati Milki za Ardhi 75 wakati wa uzinduzi rasmi wa Kliniki ya Ardhi ya Kidigiti katika uwanja wa Mashujaa Sept 25, 2026.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo Pamoja na viongozi wa wilaya ya Mtwara wakiwa katika picha ya Pamoja na wananchi waliokabidhiwa hati milki za ardhi wakati wa uzinduzi rasmi wa Kliniki ya Ardhi ya Kidigiti katika uwanja wa Mashujaa Sept 25, 2026. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Post a Comment

0 Comments